KOCHA Mkuu wa Azam FC Academy, Tom Legg, ameanza kuwafanyia tathimini wachezaji vijana wa kituo hicho ili kusuka kikosi imara.
Legg, 28, leo asubuhi alifanya mazoezi ya kwanza kwa kuwaweka pamoja vijana hao, tofauti na siku tano zilizopita za mazoezi walipokuwa wakichanganywa na wachezaji wa timu kubwa ya Azam FC.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, Legg amesema ataanza kuwafanyia tathmini wachezaji waliokuwa chini ya umri wa miaka 20 kwa muda wa wiki mbili zijazo.
"Ni mapema mno kuanza kuhukumu wachezaji, kuna baadhi wameonekana kufanya vizuri mazoezini, kuna wengine wanatakiwa kuongeza juhudi, hivyo ni mapema kwa wakati huu bado tunawafabyia tathimini, itakuwa vizuri baada ya siku chache zijazo," alisema.
Mtaalamu huyo wa soka la vijana, alisema baada ya kuwafanyia tathimini, hapo wataanza kuangalia ni wachezaji gani wamefanya vizuri, wanaotakiwa kusaidiwa na wale watakaoachwa.
"Hii itachukua muda, tutawapa fursa ya kutuvutia, kutakuwa na mechi, watafanya mazoezi ya ufiti, spidi, uwepesi, nguvu na pia baadhi ya mazoezi ya mbinu," alisema.
Aliongeza kuwa: "Baada ya hapo, tutafanya pia manadalizi ya kutengeneza timu ya chini ya umri wa miaka 17, tutaanza kutafuta wachezaji mtaani, tutaanza kuzungumza na watu kujua wachezaji pande zote za nchi hii, na kisha tutawaleta hapa na kuanza kuona kama wanakidhi vigezo tunavyotaka ndani ya academy."
Legg ambaye ana Leseni Daraja A ya ukocha kutoka Baraza la Vyama vya Soka Ulaya (UEFA), ni mzoefu wa soka la Afrika akiwa amewahi kufanya kazi katika kituo cha Craig Bellamy Foundation cha nchini Sierra Leone, pia amefanya kazi barani Ulaya, Amerika Kaskazini na Asia.
0 comments:
Post a Comment