Mkutano Mkuu wa kawaida wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) uliokuwa ufanyike Tanga ikiwamo shughuli ya uwekaji jiwe la msingi kwenye kiwanja cha TFF jijini Tanga sasa umeahirishwa kwa muda usiojulikana.
Mwishoni mwa mwezi Novemba 2015,Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) mkoa wa Ilala ulitoa agizo la kufungwa na kuchukuliwa fedha kutoka kwenye akaunti za Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) ili kulipa fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.6, sehemu kubwa ikiwa ni malipo ya kutoka kwenye mishahara (PAYE) ya makoch Jan Poulsen,Kim Poulsen, na Jacob Michelsen na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mchezo kati ya Tanzania na Brazil mwaka 2010.
Baada ya hatua hiyo TFF iliwasiliana na TRA na kuweka bayana kwamba deni la walimu (makocha) na mchezo dhidi ya Brazil lilistahili kulipwa na serikali na haikuwa sahihi kulielekeza TFF.
Aidha TFF ilieleza athari ambazo zingetokea iwapo amri hiyo (Agent Order) ingetekeleezwa kuwa ni pamoja na kusitishwa kwa ziara ya timu ya vijana chini ya miaka 15 (U15) katika nchi za Rwanda, Uganda na Kenya,
kusimama kwa program za vijana na wanawake, Mkutano Mkuu, Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Kombe la Shirikisho.
Baada ya utekelezaji wa amri hiyo kuanza TFF ilifanya kikao na TRA na makubaliano ya kufungua akaunti yakafanikiwa. Hata hivyo akaunti zilifunguliwa zikiwa hazina fedha kwa kuwa zilishapelekewa Benki Kuu (BOT) na zoezi la madai haliwezi kukamilika kwa muda mfupi.
Baada ya hali hiyo kujitokeza, TFF ilifanya kila linalowezekana kuhakikisha Mkutano Mkuu unafanyika ikiwa ni pamoja na kutafuta ufadhili toka kwa wadau wake, lakini zoezi hilo limeshindikana katika muda mfupi uliopo na hivyo Shirikisho limeamua kuahirisha Mkutano Mkuu 2015 mpaka hapo hali itakaporuhusu.
0 comments:
Post a Comment