Leicester,England.
LECEISTER City imefuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya usiku huu kuilaza Sevilla kwa mabao 2-0 katika mchezo mkali wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora uliochezwa kwenye uwanja wa King Power jijini Leicester.
Mabao yaliyoipa Leceister City ushindi huo wa kihistoria yamefungwa na nahodha Wes Morgan aliyefunga bao la kwanza na winga Marc Albrighton aliyefunga bao la ushindi na kuwafanya vijana hao wa Kocha Craig Shakespeare kufuzu kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufunga mabao 2-1 katika mchezo wa awali.
Steven N'Zonzi aliikosesha bao Sevilla katika dakika za mwisho baada ya mkwaju wake wa penati kudakwa na kipa wa Leceister City, Kasper Schmeichel. Mkwaju huo wa penati ulipatikana baada ya Schmeichel kumshika ndani ya boksi kiungo wa Sevilla,Vitolo.
Aidha katika mchezo huo ilishuhudiwa Sevilla ikilazimika kumaliza pungufu baada ya winga wake Mfaransa,Samir Nasri kuonyeshwa kadi mbili za njano kwa mchezo mbaya ikiwemo kujaribu kumpiga kichwa Jamie Vardy.
Mara ya mwisho Sevilla kucheza robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Ulaya ilikuwa ni mwaka 1958.
Katika mchezo mwingine uliochezwa huko Italia,Juventus nayo imefuzu robo fainali baada ya kuifunga Porto kwa bao 1-0 lililofungwa kwa mkwaju wa penati na Paul Dybala katika dakika ya 42 baada ya Maxi Pereira kushika mpira kwa makusudi akiwa ndani ya boksi.Pereira alionyeshwa kadi nyekundu.
0 comments:
Post a Comment