Mwandishi Wetu,Dar Es Salaam.
MACHO ya wapenzi wengi wa soka nchini wikiendi hii yatakuwa kwenye viwanja viwili nchini, lakini asilimia kubwa wanausubiria kwa hamu mtanange wa aina yake kati ya wapinzani Azam FC na Yanga, utakaofanyika keshokutwaa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Jumapili vita nyingine itahamia mkoani Kagera, pale wenyeji Kagera Sugar watakapokuwa wakiikaribisha Simba katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, mechi zote hizo zikitarajiwa kuamua hatima ya nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Wakati Azam FC iliyo nafasi ya tatu kwa pointi 44 ikiwa kwenye vita kali ya kusogelea nafasi mbili za juu kileleni, inapambana na Yanga (53) ambayo ipo kwenye mchuano mkali na Simba (55) wa kuwania taji la ligi hiyo.
Ushindi wowote wa Azam FC na Kagera Sugar, ambazo nazo zinafukuzana kuwania nafasi ya tatu, utakuwa unaziweka kwenye nafasi nzuri timu hizo kuzisogelea zaidi timu za juu na kuzitibulia mipango ya ubingwa Simba na Yanga.
Kikosi cha Azam FC kinachonolewa na Mromania Aristica Cioaba, tayari kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo huo na kimejidhatiti kuibuka na ushindi na kuendeleza vita yake ya kukusanya pointi nyingi kadiri inavyowezekana ili kutimiza lengo lake la kufukuzia nafasi mbili za juu.
Kuelekea mtanange huo mkali, mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz unakukumbusha rekodi muhimu za timu hizo mbili zilipokutana kwenye mechi zote 28 kihistoria, ambapo Azam FC imeshinda mara 10 kama Yanga huku mechi nane wakienda sare.
Dakika 630 za Azam FC
Huku ikiwa imecheza mechi saba mfululizo (sawa na dakika 630) za ligi tokea mwaka huu uanze bila kuruhusu wavu wake kuguswa, pia Azam FC imecheza na Yanga katika mechi saba mfululizo za ligi bila kupoteza, kati ya hizo ikiwa imeshinda mara mbili na michezo mitano wakienda sare.
Mara ya mwisho Azam FC kupoteza dhidi ya Yanga kwenye ligi, ilikuwa ni miaka minne iliyopita Februari 23, 2013, ikipoteza kwa kuchapwa bao 1-0, tokea hapo imekuwa ikifanya vema zaidi mbele ya Wanajangwani hao kwa mujibu wa takwimu hizo.
Upinzani wa timu hizo kwa miaka ya hivi karibuni pia umefanikiwa kudhihirishwa na matokeo ya uwanjani tokea zianze kukutana kwenye ligi kwa mara ya kwanza msimu wa 2008/2009, Azam FC ilipocheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu, mtanange huo ulifanyika Oktoba 15, 2008 na Yanga kushinda kwa mabao 3-1.
Hadi sasa ukiwa ni msimu wa tisa kukutana, timu hizo zimeshakutana mara 17 kwenye ligi, huku wakilingana kila kitu kitakwimu, Azam FC ikishinda mara tano kama Yanga, huku zikienda sare mara katika mechi saba, na pia zikiwa zimefungana mabao 25.
Kombe la Kagame (mara mbili)
Azam FC kabla ya kutwaa taji hilo mwaka juzi, iliweza kuandika rekodi ya aina yake ya kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2012 na kufika fainali iliyokutana na Yanga kabla ya kupoteza kwa kufungwa mabao 2-0.
Lakini wakati ikitwaa taji hilo la kwanza, ilirekebisha makosa na kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-3 kwenye mchezo wa robo fainali kufuatia suluhu kabla ya kwenda kubeba kombe hilo kwa rekodi inayosimama ya bila kufungwa bao lolote wala kupoteza mchezo.
Kombe la FA (ASFC)
Timu hizo zimekutana mara moja tu kwenye fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), ambayo ni mwaka jana na Yanga kushinda kwa mabao 3-1.
Wakati Didier Kavumbagu, akiifungia Azam FC bao pekee, Yanga ilijipatia mabao yake kupitia kwa Amissi Tambwe, aliyefunga mawili huku Deus Kaseke akifunga jingine.
Ngao ya Jamii (mara nne)
Azam FC imekutana na Yanga mara nne mfululizo kwenye mechi za Ngao ya Jamii zinazoashiria kufungua pazia la ligi, ambapo imeweza kutwaa taji hilo mara moja msimu huu kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya 2-2.
Wakati Yanga ikiwa imetangulia kufunga mabao mawili kupitia kwa mshambuliaji wake Donald Ngoma, Azam FC ilisawazisha yote kwa mabao ya beki Shomari Kapombe na nahodha Bocco aliyefunga kwa mkwaju wa penalti.
Katika fainali tatu za mwanzo Yanga ilishinda 1-0 (2013), 3-0 (2014) na kwa mikwaju ya penalti 8-7 kufuatia sare ndani ya dakika 90 mwaka juzi.
Mapinduzi Cup (mara tatu)
Mara zote tatu walizokutana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, Azam FC imefanikiwa kuifunga Yanga mara mbili na kutoka sare mchezo mmoja, mechi zote zikiwa ni za hatua ya makundi na mara zote ilizoibuka kidedea mabingwa hao waliweza kulitwaa taji hilo.
Kwa mara ya kwanza zilikutana mwaka 2012, Azam FC ikaibugiza mabao 3-0, shukrani kwa Kipre Tchetche, aliyefunga mabao mawili huku nahodha John Bocco 'Adebayor', akipigilia bao lingine.
Mwaka jana timu hizo zilikutana tena, safari hii zikatoka sare ya bao 1-1, Azam FC ikitangulia kufunga bao safi kupitia kwa Tchetche, aliyefunga bao lake la tatu katika michuano hiyo dhidi ya Yanga huku Vicent Bossou, akiisawazishia Yanga kwa bao lilikuwa na la utata, ambalo lilionekana halijavuka mstari.
Azam FC iliendeleza mauaji dhidi ya Yanga kwenye michuano hiyo mwaka huu baada ya kuipa kipigo kikali cha 4-0, kwa mabao ya kiufundi yaliyowekwa nyavuni na nahodha Bocco, Yahaya Mohammed, Joseph Mahundi aliyepiga shuti la umbali wa takribani mita 35 huku Enock Atta akipigilia msumari wa mwisho.
Mechi za kirafiki/hisani
Timu hizo zimekutana mara mbili kwenye mechi zisizo rasmi, zilikutana Desemba 18, 2010 katika mchezo wa kirafiki na Azam FC ikaibuka kidedea kwa ushindi wa 3-1, kwa mabao yaliyowekwa kimiani na Bocco aliyetupia mawili na marehemu Patrick Mutesa Mafisango, akitupia jingine.
Mechi nyingine walipepetana katika mchezo wa hisani wa kuchangia walemavu Desemba 20, 2011 na Azam FC kushinda tena 2-0, mabao yalisukumizwa wavuni na nyota wa zamani wa timu hiyo, Mrisho Ngassa na Gaudence Mwaikimba.
Bocco, Tchetche pacha safi
Kwa mujibu wa takwimu, pacha ya nahodha Bocco na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Kipre Tchetche, ndio imekuwa na ubora zaidi ikiwa imeweza kufunga jumla ya mabao 21 kwenye mechi zote dhidi ya Yanga.
Wakati Bocco akifunga jumla ya mabao 16 kwenye mechi zote za mashindano na kirafiki dhidi ya Yanga, Tchetche naye ametupia matano, la mwisho akifunga msimu uliopita katika sare ya bao 1-1 kabla ya kutimkia nchini Oman.
Katika mabao 16 ya Bocco, 10 amefunga Ligi Kuu, mawili Mapinduzi Cup (2012, 2017) na jingine akitupia katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwaka jana, ambao walishinda kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2, huku matatu mengine akifunga ndani ya mechi zisizo rasmi (kirafiki/hisani).
Ukiachilia mbali rekodi ya kuifunga Yanga mabao hayo, Bocco pia ameifunga mabao mengi zaidi Simba akiwa ametumbukia kwenye wavu wao mara 19 kwenye mechi mbalimbali za mashindano na zisizo rasmi (kirafiki/hisani).
0 comments:
Post a Comment