Paulinho mfungaji wa mabao matatu ya Brazil
Montevideo, Uruguay.
BRAZIL imejiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu fainali za kombe la dunia la mwaka 2018 nchini Urusi kwa nchi za ukanda wa mataifa ya Amerika Kusini (CONMEBOL) baada ya alfajiri ya leo kutoka nyuma na kuifunga Uruguay mabao 4-1 katika mchezo mkali uliochezwa huko Estadio Centenario, Montevideo,Uruguay.
Wenyeji Uruguay ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza baada ya mshambuliaji wake mahiri Edinson Cavani kufunga kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 9 ya mchezo.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha Brazil ambao walikuja juu na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 19 kupitia kwa kiungo wake Paulinho aliyekuwa nyota wa mchezo huo baada ya kufunga mabao matatu.Mabao mengine ameyafunga katika dakika za 52' na 90.Bao jingine limefungwa na Neymar katika dakika 74'.
Katika mchezo huo Uruguay iliwakosa nyota wake wawili wa kutumainiwa Luis Suarez na mlinda mlango Fernando Muslera waliofungiwa.Brazil ilimkosa majeruhi Gabriel Jesus.
Ushindi huo umeifanya Brazil iendelee kujitanua kileleni baada ya kufikisha pointi 30 katika michezo 13.Uruguay inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 23.Argentina iko nafasi ya tatu na pointi zake 22.
Katika michezo mingine:Argentina ikiwa nyumbani Buenos Aires imeifunga Chile kwa bao 1-0 lililofungwa na Lionel Messi kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 16 ya mchezo.
Colombia imeifunga Bolivia bao 1-0 shukrani kwa bao la mkwaju wa penati wa James Rodriguez katika dakika ya 83. Paraguay imeifunga Ecuador 2-1 .
0 comments:
Post a Comment