MOJA ya mashabiki wajeuri katika timu za Ligi Kuu Bara ni Yanga. Yanga wajeuri na wanajiona wako juu ya kila kitu, hawayumbishwi na yeyote yule. Haikuwa kitu cha kushitua mwaka 1977 waliposhinikiza uongozi wao kuachana na mastaa wao muhimu na kwenda kukutana na Simba kisha wakafungwa mabao 6-0. Hawa ndiyo Yanga ambao kuna wakati maamuzi yao huwa wanayaelewa wao wenyewe. Kuna wakati mwanadamu anahitaji kujielewa mwenyewe na sio kueleweka na mwanadamu mwenzie.
Hakuna kitu mashabiki wake wananiacha hoi wakati huu kama ukikutana nao viwanjani wakijikusanya vikundi vikundi na kumponda staa wao Haruna Niyonzima. Wanamponda mno mpaka unajisikia vibaya na kama una moyo mwepesi unaweza kumtafuta Haruna na kumwambia, lakini siku nyingine wakiamua kumsifu wana msifu kweli.
Hawa ndiyo Yanga ambao wakati huu wameshikwa pabaya na Haruna na wanaishia kulalama tu na sio kufanya maamuzi magumu kama waliyowahi kuyafanya 1977. Wenyewe humchukia Haruna kwenye kila mchezo wanaopoteza dhidi ya Simba. Wakishinda dhidi ya Simba na Haruna akiwa ndani ya kikosi wanakuwa wameshinda pamoja na husikii lolote lile zaidi ya sifa luluki kwa kila mchezaji. Lakini wakipoteza kila mmoja analia na Haruna na maneno mengi yatasemwa, lakini hawamfukuzi.
Stori zilizotanda sasa kwenye mitandao ya kijamii ya vyombo vya habari ni kuwa Haruna anaachwa na Yanga baada ya kusadikiwa kuwa na tabia ya kupewa mlungura na Simba ili acheze chini ya kiwango. Hizi sio stori nilizoanza kuzisikia mwaka huu, mwaka jana au mwaka juzi, ni stori za siku nyingi tu. Uzuri wa stori hii huja kuizima Haruna mwenyewe anapokuja uwanjani kufunga bao la kideoni na kila shabiki kusahau yaliyopita.
Ulahisishaji wa mpira uliotuama kwenye miguu ya Haruna unaorahisisha michezo mingi ya Yanga inayoonekana kuwa migumu yeye kuifanya miepesi, Haruna anaachwaje kwa stori za hadidu rejea? Wanaolia na Haruna hivi sasa kuwahujumu kesho ndiyo wanakuwa wa kwanza kubishana na mashabiki wenzao wa Simba kuwa ni kiungo gani mahiri kati ya Haruna na Muzamir Yassin. Siwashangai sana, siku hizi nimewazoea.
Juu ya jeuri yote waliyowahi kuwa nayo huko nyuma, lakini kwa Haruna wamekwama na wanaishia kuzungumza na baada ya mfupi wanakaa kimya na maisha mengine yanaendelea. Kama ingekuwa zamani zama za Haruna zingeshafutika siku nyingi Jangwani, lakini wakati huu unamuacha Haruna ili nafasi yake aje kucheza kiungo gani anayeweza kukifikia hata robo ya kivuli chake? Said Juma Makapu, Pato Ngonyani? Hapana! Kama jibu hapana basi tukae kimya!
Wakati Yanga wakisema wanataka kumuacha Haruna timu nyingi zimetega masikio kuona Yanga watamalizana vipi na Haruna ili zimsajili katika timu zao. Ukishakuwa na mchezaji wako ambaye anagombaniwa na timu nyingine, unamuachaje kirahisi ili aende kuimarisha nyumba ya jirani na baadae aje kukudhulu wewe mwenyewe?
Ujinga waliowahi kufanya Simba miaka ya hivi karibuni kumruhusu Ammis Tambwe kuvuka barabara yao ya Msimbazi na kuingia barabara ya Mtaa wa Twiga na Jangwani na Tambwe kuwa na rekodi nzuri ya kuwafunga Simba kila wakikutana nae, unadhani Simba hawajutii kosa hili wakijifungia ndani kwenye ofisi zao? Wanajiualimu sana tena sana, lakini hawawezi kujilaumu mbele yetu. Wanajilaumu wakiwa wenyewe.
Katika stori ya Tambwe kuachwa Simba na kuwaadhibu mara kwa mara, Yanga kwa jeuri waliyonayo hawatataka hili liwatokee kwenye upande wao kwa Haruna kuwaadhibu na wanachokifanya wakati huu ni kumpenda Haruna kisha wanachukia kumpenda. Hawana njia nyingine.
0 comments:
Post a Comment