Bakayoko kulia mwenye nywele nyeupe |
Paris,Ufaransa.
KOCHA wa timu ya taifa ya Ufaransa,Didier Deschamps,amemuita kwa mara ya kwanza kwenye kikosi chake kiungo mahiri wa Monaco,Tiemoue Bakayoko kuziba pengo la Paul Pogba anayesumbuliwa na majeruhi tayari kwa michezo miwili ya kimataifa dhidi ya Luxembourg na Hispania.
Pogba,24,aliumia misuli siku ya Alhamisi wakati akiichezea Manchester United kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rostov ya Urusi kwenye michuano ya kombe la Europa Ligi na anatarajiwa kuwa atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha siku 15.
Kadhia hiyo imemfanya Deschamps kumwona Bakayoko,22,kama mbadala sahihi wa Pogba. Ikumbukwe Bakayoko alikuwa hajawahi kuitwa kwenye kikosi cha wakubwa cha Ufaransa.
Mapema wiki hii Bakayoko aligonga vichwa vya habari vya kimataifa baada ya kuifungia Monaco bao la ushindi lililoisukuma Manchester City nje ya michuano ya klabu bingwa Ulaya.
Bakayoko anakuwa mchezaji wa tano wa Monaco kuitwa kwenye kikosi cha Deschamps.Wengine ni Djibril Sidibe,Benjamin Mendy, Thomas Lemar na Kylian Mbappe.
Machi 25 mwaka huu Ufaransa itasafiri kwenda kuivaa Luxembourg kwenye mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki kombe la dunia la mwaka 2018.Siku tatu baadae Ufaransa itakuwa nyumbani Parc des Princes kuialika Hispania kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki.
0 comments:
Post a Comment