Lilongwe,Malawi.
MALAWI imetangaza kuwa itashiriki kinyang'anyiro cha kusaka tiketi ya kufuzu fainali za michuano ya Afrika (AFCON 2019) ikiwa ni siku nne zimepita tangu itangaze kujitoa kwenye michuano hiyo kutokana na kukabiliwa na ukata mkali wa kifedha.
Mapema wiki hii chama cha soka cha Malawi (FAM) kilitangaza kuitoa timu hiyo kwenye michuano yote ya ndani ya Afrika kutokana na kukosa fedha za maandalizi pamoja na kuajiri kocha wa kigeni kwa madai kuwa serikali ya nchi hiyo ilikataa kuchangia asilimia hamsini ya gharama za kutekeleza mipango hiyo.
Leo Jumamosi FAM kupitia kwa afisa wake,Walter
Nyamilandu imesema Malawi imeamua kushiriki michuano ya Afcon na ile ya Chan baada ya serikali ya nchi hiyo kuahidi kukipatia chama hicho fedha za kutosha.
Malawi imepangwa kucheza na Madagascar katika mchezo wake wa awali wa kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya wachezaji wa ndani (CHAN 2018).Mchezo huo utachezwa Aprili mwaka huu.
Baadae Malawi itavaana na mshindi kati ya Comoros na Ushelisheli katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya AFCON ya mwaka 2019.Mchezo huo umepangwa kufanyika Juni 13 mwaka huu .
0 comments:
Post a Comment