Birmingham, England.
ARSENAL imeendelea kujitengenezea mazingira magumu ya kumaliza katika nafasi nne za juu ligi kuu England baada ya mchana wa leo kufungwa mabao 3-1 na West Bromwich Albion katika mchezo uliochezwa kuanzia mishale ya 9:30 kwenye uwanja wa Hawthorns huko jijini Birmingham.
Wenyeji West Bromwich Albion ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza baada ya beki wake wa kulia,Craig Dawson kufunga kwa kichwa katika dakika ya 12 akiunganisha kona ya Nacer Chadli.
Dakika tatu baadae yaani katika dakika ya 15 Alexis Sanchez aliirudisha Arsenal mchezoni baada ya kufunga bao la kusawazisha akiunganisha pasi ndefu ya Granit Xhaka na kufanya mchezo uende mapumziko matokeo yakiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza mapema kuiendea kombo Arsenal baada ya kipa wake namba moja Peter Cech kuumia nyonga na kutoka uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na David Ospina.
West Bromwich Albion walipata bao la pili katika dakika ya 52 baada ya mtokea benchi Robinson Kanu kuuwahi mpira uliomshinda kipa wa Arsenal,David Ospina na kuutia kimiani.Craig Dawson kwa mara nyingine aliwanyanyua vitini mashabiki wa Westbrom baada ya kufunga bao la tatu kwa kichwa katika dakika ya 72 na kufanya Arsenal ilale kwa mabao 3-1.
0 comments:
Post a Comment