Dar es salaam,Tanzania.
Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara Yanga wameendelea kuonyesha nia ya kuutetea ubingwa wao baada ya jioni ya leo kuichapa Mwadui FC mabao 2-1 katika mchezo mkali uliopigwa katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza baada ya winga Simon Msuva kufunga kwa kichwa dakika ya 3 tu ya mchezo akiunganisha krosi ya mlinzi wa kushoto Oscar Joshua.
Dakika ya kumi baadae yani dakika ya 13 mshambuliaji Kelvin Sabati aliifungia Mwadui FC bao la kusawazisha baada ya kuunasa mpira uliomponyoka kiungo wa Yanga Thabani Kamusoko.
Mpaka mapumziko matokeo yalikuwa 1-1,Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kucheza kwa tahadhari kubwa huku zikikosa mabao ya wazi.
Yanga ilifanikiwa kupata bao la ushindi dakika ya 86 kupitia kwa kiungo wake Haruna Niyonzima aliyefunga kwa mkwaju mkali baada ya kupokea pasi ya kichwa toka kwa Donald Ngoma.
Kufuatia matokeo hayo Yanga imefikisha pointi 56 ikiwa ikiwa na michezo 23 pointi moja nyuma ya vinara Simba SC wenye pointi 57 baada ya kucheza michezo 24.
Katika mchezo mwingine Azam FC imeifunga Mtibwa Sugar 1-0 kwa bao la mkwaju wa penati wa nahodha John Bocco uliopatikana baada ya Kipre TcheTche kuangushwa kwenye eneo la hatari la Mtibwa Sugar.
Sasa Azam FC imefikisha pointi 55 baada ya kushuka dimbani mara 24.
0 comments:
Post a Comment