Barcelona,Hispania.
Barcelona imeendelea kujitengenezea mazingira magumu ya kutetea ubingwa wake wa Ligi ya La Liga baada ya leo usiku kuchapwa mabao 2-1 na Valencia nyumbani Camp Nou na kuweka rekodi ya kupoteza michezo mitatu mfululizo ya Ligi tangu mwaka 2003.
Barcelona ikiwa bado haijapona maumivu ya kuvuliwa ubingwa wake wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ilijikuta ikiwa nyuma kwa bao moja dakika ya 26 tu ya mchezo baada ya kiungo wake Ivan Rakitic kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa krosi ya Guilherme Siqueira.
Ikiwa hiyo haitoshi dakika ya 45 krosi ya Dani Parejo ilimkuta Santi Mina akiwa katika nafasi nzuri na kuifungia Valencia bao la pili kwa mkwaju mkali.
Lionel Messi alimaliza ukame wa kutofunga bao katika michezo mitano mfululizo baada ya kuifungia Barcelona bao la kufutia machozi dakika ya 64 akipokea pasi ya mlinzi wa kushoto Jordi Alba.Hilo linakuwa ni bao la 500 la nyota huyo kufunga katika maisha yake ya soka.
Kufuatia kichapo hicho Barcelona bado iko kileleni ikiwa na pointi 76 sawa na Atletico Madrid huku Real Madrid ikiwa ya tatu na pointi zake 75,Valencia wao wamepanda mpaka nafasi ya 12 baada ya kufikisha pointi 40 katika michezo 33.
0 comments:
Post a Comment