Milan,Italia.
Ndoto za Napoli kuendelea kuipa presha Juventus kileleni katika kinyang'anyiro cha kuusaka ubingwa wa Ligi ya Seria A zimekwaa kigingi baada ya jana usiku kukubali kichapo cha mabao 2-0 toka kwa Inter Milan katika mchezo mkali uliopigwa huko Giusseppe Meaza,Milan.
Inter Milan ikitumia vyema pengo la Napoli kumkosa mshambuliaji wake Gonzalo Higuain aliyefungiwa ilijipatia bao la kuongoza kupitia kwa nahoda wake Mauro Icardi baada ya kupokea pasi ndefu ya kiungo Gary Medel na kumfunga kirahisi mlinda mlango Pepe Reina.
Dakika chache kabla ya mapumziko Inter Milan ilipata bao la pili kupitia kwa kiungo Marcelo Brozovic aliyeiwahi pasi ya Mauro Icardi na kuamsha shangwe Giusseppe Meaza.
Kufuatia ushindi huo Inter Milan imefikisha pointi 61,pointi tatu nyuma ya AS Roma yenye pointi 64,Napoli iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 70.Juventus wao wako kileleni wakiwa na pointi 76 huku jioni ya leo wakiwa nyumbani kuikaribisha Palermo.
0 comments:
Post a Comment