Sagrada Esperanca
Dar es salaam,Tanzania.
KAZI ya kuwaua Waangola katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, imeanza kwa mabingwa wa soka Tanzania, Yanga baada ya timu hiyo ya Jangwani kunasa siri za wapinzani wao,Grupo Desportivo Sagrada Esperanca ya Angola.
Yanga imeangukia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 bora ya Klabu Bingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2.
Baada ya kufanyika kwa droo na kupangwa na timu hiyo ya Angola, Yanga walianza mkakati wa kuichunguza timu hiyo mapema kabisa na sasa tayari wamepata mikanda ya timu hiyo katika mechi zake mbalimbali.
“Tumepata mikanda ya wapinzani wetu na itakabidhiwa kwa benchi la ufundi kwa ajili ya hatua muhimu za kuwasomba mbinu zao na mambo mengine,”alisema mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye hata hivyo hakupenda kutajwa jina lake kwa madai si msemaji.
Alisema kuwa wamefanikiwa kupata mikanda ya mechi kadhaa ikiwemo mchezo wao wa mwisho wa Kombe la Shirikisho dhidi ya V.Club Makonda ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambapo Waangola hao walishinda kwa mabao 2-1.
Yanga itakutana na G. D. S. Esperanca Mei 6,katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kufanyika kati ya Mei 16 na 17 jijini Luanda nchini Angola.
Yanga inajipanga kupata ushindi katika mchezo wa kwanza, ili kujiweka katika
mazingira mazuri ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Kwa upande wake kocha wa Yanga, Hans Van der Pluijm, alisema hawafahamu wapinzani wake hao, lakini itakuwa ni jambo la heri kwa benchi lake la ufundi kupata mikanda itakayowawezesha kuwasoma wapinzani wao kabla ya mchezo huo.
Chanzo:Bingwa
0 comments:
Post a Comment