Dar es salaam,Tanzania.
KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja,amewachambua wachezaji wake wawili, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Ramadhan Kessy anayeamini kuna watu wanaompotosha ambao ni wazi wanamharibia kipaji na maisha yake kwa ujumla.
Akizungumza Mayanja ambaye amekikimbizia kikosi chake Zanzibar kwa ajili ya kambi ya kujipanga na mechi zao tano zilizobaki za Ligi Kuu Tanzania Bara,pia alimwelezea Mgosi kama mchezaji anayevutiwa mno kufanya naye kazi.
Juu ya Mgosi, Mayanja alisema kuwa anaweza kuwa kocha mzuri wa Simba kwa siku za baadaye kutokana na nidhamu kubwa aliyonayo na usikivu.
“Mgosi ni aina ya wachezaji ambao walikuwa hazina kubwa kwa taifa kama ningekuwa Kocha Mkuu wa Simba ningependa kufanya naye kazi akiwa msaidizi wangu,” alisema Mayanja.
Aliongeza hivi sasa Mgosi ni kocha mchezaji katika kikosi hicho lakini mara nyingi amekuwa akifanya naye kazi kwa karibu na kupeana ushauri katika mambo mbalimbali ya kiufundi yanayohusu Simba.
Mayanja alisema bado anatambua kuwa yeye bado kocha msaidizi wa Simba na endapo atapata barua rasmi ya kupewa mikoba ya kocha mkuu angependa kufanya kazi na Mgosi akiwa msaidizi wake.
“Mgosi amecheza muda mrefu soka, anajua fitina za soka la Tanzania, lakini pia ni mzoefu wa saikolojia za wachezaji wa ndani,anaweza kumudu kuwa kocha kwa siku za baadaye,” aliongeza Mganda huyo.
Kuhusiana na Kessy, kocha huyo alisema kuwa beki wao huyo wa kushoto ambaye kwa sasa amesimamishwa mechi tano, amesema wajanja wachache wanamdanganya mchezaji
huyo.
“Siku hizi kumeibuka mawakala feki wa wachezaji utakuta anatumia fedha nyingi kujifanya wakala wa mchezaji fulani akijua kufanya hivyo kuna faida ataipata mbeleni,hii ni mbaya sana,” alisema Mayanja.
Aliongeza kuwa Kessy anadanganywa na watu wachache walio nyuma yake na kumfanya mchezaji huyo kukosa nidhamu na kufanya vituko mbalimbali katika timu hiyo.
“Mimi nilikaa naye na kumwambia mambo mengi kama ataendelea na staili hii ni wazi hana muda mrefu katika maisha yake ya soka. Kwa sasa yupo katika kiwango cha juu kuna watu wachache wanajifanya mawakala wake wanamdanganya, ngoja tuone mwisho wake,” aliongeza.
Alisisitiza kuna wachezaji wengi Ligi Kuu wenye uwezo mkubwa kuliko Kessy, lakini hawapati nafasi ya kuzichezea Simba au Yanga, wakiwa wanazitamani.
“Angalia kwa umakini sana hata kama ataenda Yanga au Azam atacheza wapi?Alihoji Mayanja.
Chanzo:Bingwa
0 comments:
Post a Comment