Paris,Ufaransa.
Manchester City imejiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa mara ya kwanza nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya baada ya jana usiku kuibana Paris Saint-Germain na kutoka nayo sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza wa robo fainali uliopigwa Parc des Princes jijini Paris.
Manchester City ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 38 kupitia kwa winga wake Mbelgiji Kevin De Bruyne aliyemalizia pasi nzuri ya Fernando aliyempokonya mpira Blaise Matuidi.
Dakika tatu baadae yaani dakika ya 41 mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic aliifungia Paris Saint-Germain bao la kusawazisha akitumia makosa ya kiungo Fernando aliyeshindwa kuanzisha vizuri mpira wa goal kick.
Kipindi cha pili kiungo Adrien Rabiot alipatia Paris Saint-Germain bao la pili akiuwahi mpira uliotemwa na mlinda mlango wa Manchester City Hart uliotokana na kichwa kikali cha Edinson Cavani.
Dakika ya 72 kiungo Fernando Luiz Rosa aliifungia Manchester City bao la kusawazisha baada ya walinzi wa Paris Saint-Germain Serge Aurier na Thiago Silva kuchelewa kuucheza mpira wa krosi wa mlinzi Bakari Sagna.
Katika mchezo mwingine wa ligi ya Mabingwa,Real Madrid imeangukia pua baada ya kufungwa mabao 2-0 na Wolfsburg huko Volkswagen Arena.
Ricardo Rodriguez aliifungia Wolfsburg bao la kuongoza dakika ya 18 kwa mkwaju wa penati uliopatikana baada ya Casemiro kumwangusha katika eneo la hatari mshambuliaji Andre Schurrle.
Bao la pili limefungwa na Maximilian Arnold dakika ya 25 baada ya kupokea pasi toka kwa Henrique na kumfunga kirahisi mlinda mlango wa Real Madrid Kylor Navas.
Michezo ya mkondo wa pili wa hatua ya robo fainali itachezwa jumanne ijayo
0 comments:
Post a Comment