Lusaka,Zambia.
TIMU ya taifa ya vijana ya Zambia ya vijana wa chini ya umri wa miaka 20 imetinga fainali ya Afrika ya michuano ya Afcon ya vijana wa umri huo ya baada ya jana Jumatano jioni kuilaza Afrika Kusini kwa bao 1-0 katika mchezo mkali wa nusu fainali uliochezwa katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa,jijini Lusaka-Zambia.
Bao pekee la mchezo huo ulioshindwa kumpata mshindi ndani ya dakika tisini za kawaida limefungwa kwa kichwa na Edward Chilufya katika dakika ya 108.
Zambia ilifanikiwa kutinga nusu fainali baada ya kumaliza ikiwa kinara wa kundi A.Ikijikusanyia pointi tisa huku katika mchezo wake wa mwisho ikiifunga Misri na kuipeperushia ndoto za kufuzu michuano ya kombe la dunia la vijana la mwaka 2017.
Afrika Kusini ilimaliza nafasi ya pili katika msimamo wa kundi B.Ikijikusanyia pointi sita ikizifunga Cameroon na Sudan kabla ya kufungwa na Senegal.
Kwa ushindi huo sasa ina maana kwamba Zambia itacheza fainali na mshindi wa leo kati ya Senegal na Guinea.Ikumbukwe pia kuwa timu zote nne zilizofuzu nusu fainali zimepata tiketi ya kushiriki fainali ya kombe la dunia la vijana wa umri wa miaka 20 litakalofanyika Korea Kusini kati ya Mei 20 -Juni 11.
0 comments:
Post a Comment