Mbeya,Tanzania.
KOCHA
Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben
Hernandez, amepongeza ari ya kupambana iliyonyeshwa na wachezaji wake
katika mechi zote mbili za mkoani Mbeya, huku akidai kuwa sasa mafunzo
yao yameanza kuzaa matunda ndani ya kikosi hicho.
Hiyo inatokana na kikosi cha Azam FC jana kukamilisha mechi zake
mbili za mkoani Mbeya kwa kuzoa pointi zote sita, hasa baada ya ushindi
dhidi ya Mbeya City (2-1) na ule wa kihistoria walioifunga Tanzania
Prisons bao 1-0.
“Nawashukuru wachezaji kwa sababu mafunzo ambayo wamepokea tokea
kipindi tunakuja yanaonekana yanazaa matunda kwa sababu kupata pointi
sita ugenini hasa Mbeya ilikuwa ni kama historia.
“Lakini kiukweli kwa sasa hivi imekuwa ni kama kazi rahisi kwa sababu
vijana wamejituma sana, na tulichowafundisha ndicho walichoenda
kukitekeleza,” alisema.
Aliongeza kuwa : “Kazi imekuwa kubwa sana kwa sababu mpira ambao sisi
kama makocha tulitegemea uchezwe, sio ule ambao umechezwa ukilinganisha
na hali ya uwanja, lakini pia aina ya mazingira ambayo tumeweza
kukutana nayo, ambayo yote ni tofauti sana na yale ambayo tumeyazoea
Chamazi.”
Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, pia alichukua fursa
hiyo kuwaelezea wachezaji wapya wa kikosi hicho walioanza kuichezea
Azam FC jijini hapa, beki Daniel Amoah na mshambuliaji Gonazo Bi Thomas,
akisema kuwa ni wachezaji wazuri.
“Ni wachezaji ambao nao wameonyesha uwezo wao, mazoezi waliyokuwa
wakiyapata ingawa kwa kipindi kifupi wamejaribu kuyafanyia kazi,
ingawaje kwa wao kazi imekuwa ni ngumu kidogo na hii ni kwa sababu bado
hawajaweza kuzoeana na wenzao,” alisema.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB itashuka tena dimbani Septemba 17 mwaka huu kuvaana na Simba.
0 comments:
Post a Comment