728x90 AdSpace

  • Latest News

    Wednesday, September 21, 2016

    MPIRA WA AFRIKA BADO UNA SAFARI NDEFU SANA KUFIKIA MAFANIKIO


    Paul Manjale.

    UNAWEZA ukastaajabu uwezavyo.Ukatahamaki uwezavyo.Ukasema chochote utakacho lakini ukweli ukabaki pale pale kuwa mpira wa Afrika bado una safari ndefu sana mpaka kufikia mafanikio ya juu waliyofikia wenzetu wa Ulaya na kwingineko.

    Hakuna asiyejua kuwa Afrika imejaliwa kuwa na vipaji maridhawa katika soka,riadha na michezo mingine.Lakini hebu jiulize kwanini mpaka leo Afrika haijawahi kufika japo hata nusu fainali ya kombe la dunia achilia mbali kulitwaa.

    Leo hii mchezaji ghali zaidi duniani Paul Pogba asili yake ni Afrika.Pele,Ronaldinho,Zinedine Zidane hawa nao asili zao ni hapa hapa Afrika.Lakini licha ya vipaji vyote hivi unagundua kuwa Afrika imekosa kitu kimoja tu,uongozi makini.

    Hivi karibuni timu ya taifa ya soka ya wanaume ya Nigeria ya U-23 ilifanikiwa kumaliza katika nafasi ya tatu ya michuano ya Olimpiki iliyofanyika nchini Brazil na kufanikiwa kujinyakulia medali ya shaba.

    Lakini ukiambiwa kilichokuwa kinaikumba kambi ya timu hiyo iliyokuwa Atalanta,Marekani unaweza ukamwaga chozi.

    Hivi utaamini ukiambiwa kuwa wachezaji wa Nigeria walikuwa wakishinda njaa,wakikosa usafiri wa kwenda na kurudi mazoezini,hawakuwa na uwanja wa kufanyia mazoezi wala fedha za kujikimu??

    Hivi utaamini kuwa nahodha wake John Obi Mikel ndiye aliyekuwa akitoa pesa ya chakula kwa wachezaji wenzie?ndiye aliyekuwa akikodi basi kwa ajili ya kwenda na kurudi mazoezini.Pia inasemekana ndiye aliyefanikisha timu ikasafiri mpaka Brazil baada ya viongozi kuchemsha kupata usafiri wa ndege.

    Hiyo ndiyo hali halisi ya namna kambi ya Nigeria ilivyokuwa huko Atalanta,Marekani.Maisha yalikuwa magumu na ndiyo maana haishangazi kusikia kuwa timu iliwasili Brazil masaa machache kabla ya mchezo wake wa kwanza.

    Swali la kujiuliza hapa Je,Nigeria ilikwenda Atalanta kufanya nini?!Kama ni kambi kwanini isingeweka nyumbani wachezaji wakawa wanatokea majumbani kwao.Badala ya kugeuka omba omba katika mitaa ya jiji la Atalanta?

    Hayo yote yaliyotokea kwenye kambi ya Nigeria.Yanayotokea Tanzania na kwingineko Afrika.Hii ni uthibitisho tosha kuwa soka la Afrika limekosa viongozi makini.Viongozi ambao watatutoa hapa tulipo na kutupeleka kule tunakotamani kufika.

    Hebu jiulize kama Nigeria ingepata maandalizi mazuri.Wachezaji wangepewa mahitaji yao kwa wakati,unadhani ile medali ya dhahabu ingebaki Brazil?Thubutu kwa jeuri gani waliyonayo Wabrazil siku hivi?

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: MPIRA WA AFRIKA BADO UNA SAFARI NDEFU SANA KUFIKIA MAFANIKIO Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top