Dar Es Salaam,Tanzania.
Shirikisho la Soka nchini, TFF limewateua waamuzi watakaosimamia pambano la kwanza la watani wa jadi la msimu huu likalopigwa siku ya Jumamosi katika dimba la Taifa.
Mwamuzi Martin Saanya amekabidhiwa jukumu la kupuliza filimbi katika hio inayogusa hisia za watanzania wengi.
Mwamuzi huyo si mgeni wa mechi kubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Msimu uliopita alipewa jukumu kubwa la kuamua mechi ya Ngao ya Jamii baina ya Yanga na Azam na kuitendea haki ipasavyo.
Msimu wa 2014/15 Saanya alichezesha mechi ya watani wa jadi ambayo Simba ilifanikiwa kuidungua Yanga kwa bao 1-0 lililotoka katika miguu ya Emmanuel Okwi.
Saanya mwenye beji ya FIFA anakumbukwa zaidi kwa kufungiwa kuchezesha soka kwa kipindi cha mwaka mmoja na uongozi uliopita wa TFF baada ya kutuhumiwa kutochezesha vizuri mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Costal Union ambayo matokeo yake yalimalizika kwa sare ya mabao 1-1 mnamo msimu wa 2013/14.
Hata hivyo mara tu Rais wa sasa wa TFF, Jamal Malinzi alipoingia madarakani alimtoa Saanya kifungoni mara moja yeye pamoja na waamuzi wengine waliofungiwa.
Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha watamsaidia Saanya kwa kuwa washika vibendera. Wkati huo huo, kiingilio cha chini katika pambano hilo kimepangwa kuwa Shilingi 7000. Viingilio vingine ni shilingi 10,000, 20,000 na 30,000.
0 comments:
Post a Comment