Berlin, Ujerumani.
ANDRE Schurrle (Pichani) akishangilia baada ya kuifungia klabu yake ya Borussia Dortmund bao la kusawazisha na kuiwezesha kutoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Real Madrid katika mchezo mkali wa kundi F wa ligi ya mabingwa Ulaya uliochezwa usiku huu katika uwanja wa Signal Iduna Park huko Berlin Ujerumani na kushuhudiwa na watazamaji 64,849.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Mwamuzi,Mark Clatternberg,kutoka Uingereza ilishuhudiwa Real Madrid ikipata bao la kuongoza dakika ya 17 ya mchezo kupitia kwa Cristiano Ronaldo.
Bao hilo halikudumu sana kwani mnano dakika ya 43 Emerick Aubameyang aliifungia Borussia Dortmund bao la kusawazisha baada ya kipa wa Real Madrid Keylor Navas kushindwa kuondosha vyema hatari katika lango lake na kufanya matokeo yawe sare ya 1-1 mpaka mapumziko.
Kipindi cha pili walikuwa ni Real Madrid tena ndio waliotangulia kupata bao la pili dakika ya 68 ya mchezo kupitia kwa beki wake Mfaransa,Raphael Varane.Varane alifunga bao hilo akimalizia pasi ya Karim Benzema.
Mchezo ukiwa unaelekea ukiongoni Andre Schurrle aliifungia Borussia Dortmund bao kusawazisha dakika ya 87 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Ivan Pulisic na kufanya mchezo umalizike kwa sare ya mabao 2-2.
Sare hiyo imeinyima Real Madrid kushinda japo mchezo mmoja nyumbani kwa Borussia Dortmund kwani katika michezo sita iliyocheza Signal Iduna Park imeambulia sare mara tatu na kufungwa mara tatu.
0 comments:
Post a Comment