728x90 AdSpace

  • Latest News

    Tuesday, September 27, 2016

    SIRI IMEFICHUKA:SABABU YA AZAM FC KUCHECHEMEA LIGI KUU BARA HII HAPA


    Dar Es Salaam,Tanzania.

    BAADA ya Azam FC kupoteza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara,imedaiwa kuwa moja ya vitu vilivyosababisha kupoteza morali kwa wachezaji wao ni kukosa posho tangu kuanza kwa msimu huu.

    Tangu kuanza kwa ligi msimu huu, Azam imekuwa na mwendo wa kinyonga jambo ambalo limesababisha kujikuta wakipata matokeo yasiyoridhisha kwenye mechi zake.

    Katika michezo sita waliyocheza hadi sasa,Azam imeshinda mechi tatu, sare moja na kupoteza mara mbili, ambapo ilianza ligi dhidi ya Africans Sports na kupata sare ya 1-1, ikaifunga Majimaji 3-0, ikaitandika pia Tanzania Prisons 1-0, ikapata ushindi wa 2-1 mbele ya Mbeya City, lakini ikajikuta ikinyukwa 1-0 dhidi ya Simba kabla ya juzi kutandikwa 2-1 na Ndanda FC.

    Kwa matokeo hayo, Azam imejikuta ikishika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 10 sawa na Tanzania Prisons pamoja na Yanga waliocheza mechi tano.

    Taarifa zilizopatika kutoka ndani ya klabu ya Azam kupitia wanandinga wake ambao hawakutaka kutajwa majina zinadai kuwa tangu kuanza kwa ligi msimu huu,Azam wameamua kuuondoa utaratibu wa kuwapa posho wachezaji wao na badala yake wanaishi kupitia mishahara pekee.

    Taarifa hizo zinaongeza kuwa licha ya kupewa mishahara yao kwa wakati, lakini maisha ya sasa ni vigumu kuyaendesha kwa kutegemea kipato hicho ambacho wanandinga hao wanapokea huku kila mmoja akiwa na kiwango chake.

    “Zamani tulikuwa tukipewa posho, mishahara lakini pia kuna zawadi ndogo ndogo na fedha ambazo tulikuwa tukipewa kama motisha pindi tunapofanya vizuri na hiyo tuliahidiwa na mabosi zetu.

    “Lakini msimu huu hali imekuwa kinyume baada ya kubadili mfumo kwa kuamua kuondoa suala la posho na kubakisha mishahara au ahadi iwapo kama bosi yeyote atajitokeza kufanya hivi, hali hii inatufanya tusicheze kiufanisi kwani maisha ya

    kutegemea mshahara ni magumu licha ya kwamba tunalipwa kwa wakati,” alisema mwanandinga huyo tegemeo kwenye kikosi cha Wanalambalamba hao.

    Mwanandinga mwingine wa timu hiyo alisema Azam kila mchezaji ana kiwango chake cha mshahara, wapo wanaopokea fedha nyingi lakini pia wapo wale ambao fedha wanazozipata hazikidhi mahitaji yao.

    “Hapa kila mmoja na kiwango chake cha mshahara, bora yule anayepokea fedha nyingi kuliko mwenzangu na mimi ambaye mshahara wake kwanza haukidhi mahitaji hivyo siku zote alikuwa akitegemea posho kuyabeba maisha yake, hii leo imeondolewa unafikiri ataweza kuendana na ugumu wa maisha uliopo hivi sasa, ndio ile tunacheza katika kiwango katika tarehe maalumu ambazo tunakuwa na fedha mfukoni.”



    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: SIRI IMEFICHUKA:SABABU YA AZAM FC KUCHECHEMEA LIGI KUU BARA HII HAPA Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top