Orkney,Afrika Kusini.
Free State Stars ya Afrika Kusini inayochezewa na mshambuliaji wa zamani wa Simba SC Mganda,Hamis Kiiza 'Diego,imeendelea kufanya vibaya katika michezo ya ligi kuu ya nchi hiyo (PSL) baada ya Jumatano Usiku kushuhudiwa ikipoteza mchezo wake wa tatu pale ilipokubali kuchapwa mabao 2-0 na Kaizer Chiefs katika uwanja wake wa nyumbani wa James Motlatsi Stadium.
Katika mchezo huo ambao Hamis Kiiza alicheza kwa dakika 67 kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Armand Ella ilishuhudiwa Kaizer Chiefs wakiandika bao la kwanza dakika ya 10 kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Mzimbabwe, Willard Katsande.
Mkwaju huo ulipatikana baada ya Joseph Okumu wa Free State Stars kumwangusha ndani ya boksi Sibusiso Khumalo aliyekuwa amebakiza mita chake kumfikia mlinda mlango Thela Ngobeni.
Kaizer Chiefs iliandika bao lake la pili dakika ya 64 ya kipindi cha pili kupitia kwa Mzimbabwe,Michelle Katsvairo.Ushindi huo umeipeleka Kaizer Chiefs kileleni mwa msimamo wa PSL baada ya kufikisha pointi kumi katika michezo yake mitano sawa na Golden Arrows inayoshilia nafasi ya pili.
Nafasi ya tatu,nne na tano inashikiliwa na vilabu vya Orlando Pirates, Polokwane City na Cape Town City ambavyo vyote vina pointi nane nane kila kimoja.Free State Stars imeshuka mpaka nafasi ya kumi na nne baada ya kuambulia pointi mbili pekee katika michezo yake mitano.
0 comments:
Post a Comment