London, Uingereza.
LILE pambano la masumbwi la marudiano la uzito wa juu duniani lililokuwa lichezwe Octoba 29 mwaka huu kati ya bingwa wa mkanda wa WBA na WBO Mwingereza Tyson Fury na Mukraine Wladimir Klitschko limeahirishwa kwa mara nyingine.
Sababu ya kuahirishwa kwa pambano hilo zimedai kuwa Fury amepata majeraha wakati akijifua tayari kwa mpambano huo unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa masumbwi duniani kote.
Hii ni mara ya pili kwa Pambano hilo kuahirishwa.Mara ya kwanza lilipangwa kufanyika Julai 9 mwaka huu lakini lililazimika kuahirishwa baada ya Fury kuumia kifundo cha mguu.
Mpaka sasa hakuna mtu yoyote kutoka katika kambi ya Fury aliyepatikana kuzungumzia suala hilo,lakini taarifa zinasema leo asubuhi kambi ya Klitschko ilifahamishwa kuhusu kuahirishwa kwa pambano hilo.
Kuahirishwa kwa mara ya pili kwa mpambano huo kunamweka Fury katika hatari ya kupokonywa mikanda yake hiyo.
Ikumbukwe sheria za mchezo wa masumbwi zinatoa haki kwa bondia kupokonywa mikanda yake ikiwa atashindwa kuitetea ndani ya kipindi cha miezi 12 tangu alipocheza pambano lake la mwisho.
0 comments:
Post a Comment