Na Chikoti Cico.
Manchester United inapitia kwenye wakati mgumu kwasasa baada ya vipigo vitatu mfululizo walivyovipata ndani ya wiki mbili kutoka kwa Manchester City, Feyenoord na Watford, vipigo hivyo vimeleta hali ya sintofahamu ndani ya klabu hiyo na hasa kwa kocha mpya wa klabu hiyo Jose Mourinho.
Makala haya itaangalia nini hasa ambacho kwa namna moja ama nyingine kinasababisha timu hiyo kukosa mwelekeo mzuri mwanzoni kabisa mwa msimu wa 2016/17 huku mashabiki wa klabu hiyo wakianza kupata wasiwasi na mwenendo mzima wa timu yao.
Jambo ambalo linaonekana kuwa kiini cha mvurugano ndani ya Manchester United kwasasa ni Jose Mourinho kukosa kujua kipi hasa ni kikosi chake mahiri, unaweza kusema mpaka sasa kocha huyo “HAJUI KIKOSI CHAKE CHA KWANZA NI KIPI?
Hili ni jambo zito zaidi kwa Mourinho kwasababu ktk miaka yake yote aliyofundisha hasa klabu ya Chelsea, kocha huyu amekuwa na wachezaji 11 anaowaamini ambao wakati wote ndiyo huanza, ije mvu ama lije jua lazima wachezaji hao 11 waanze kwenye mchezo wowote ule. Ukiachilia mbali pale ambapo mchezaji wa kikosi cha kwanza anapoumia ama kuonyeshwa kadi nyekundu.
Mfano mzuri ni wakati akiifundisha klabu ya Chelsea, eneo la nyuma karibia wakati wote kipa alikuwa ni Cech, mabeki ni Ivanovic, Azpilicueta, Terry na Cahill, eneo la katikati ni Fabregas, Matic na Oscar, pembeni ni Willian na Hazard huku mbele akicheza Costa. Na hawa ndiyo waliompa Mourinho ubingwa msimu wa 2014/15.
Na kama ukiangalia takwimu za wachezaji hao wa Chelsea kwa mechi walizokosa ni chache mno huku wengi wao ikiwa ni baada ya kusimamishwa na FA ama kuumia uwanjani kwa kipindi chote cha msimu wa 2014/15 mpaka walipotwaa ubingwa wa ligi ya primia.
Ukiangalia kwasasa ndani ya Manchester United ni kama vile Mourinho bado yuko kwenye mazoezi ya kujiandaa na msimu wa ligi yaani “pre season” kwasasababu mpaka sasa kocha huyo ni kama hajui kikosi chake cha kwanza ni kipi na ni kama mpaka sasa anafanya majaribio ya wachezaji.
Tuangalie mifano michache, katika michezo mitatu ya ligi ambayo United walicheza na kushinda, ikiwa ni dhidi ya Bournemouth, Southampton na Hull City , michezo yote hiyo kiungo Juan Mata alianza kwenye kikosi cha kwanza.
Mchezo uliofuata dhidi ya Manchester City Mata akaanzia benchi, akarejeshwa kwenye kikosi cha kwanza wa EUROPA dhidi ya Feyenoord na kutupwa benchi tena kwenye mchezo wa ligi dhidi ya primia dhidi ya Watford. Ukiangalia kwa ukaribu hii sio namna ambavyo Mourinho huendesha timu yake.
Mfano mwingine ni eneo la beki wa katikati, kwenye michezo minne ya ligi Blind na Bailly ndiyo walioaminika na kuonekana kwamba wana uwezo wa kuibeba United kwenye eneo la ulinzi lakini baada ya mabeki hawa kuvurunda kwenye mchezo dhidi ya Manchester, mchezo uliofuata dhidi ya Feyenoord kwenye ligi ya EUROPA Blind akaanzia benchi na nafasi yake kuchukuliwa na Smalling vivyo hivyo kwenye wa primia dhidi ya Watford, hali ambayo inakufanya ujiulize Mou anataka nini hasa.
Naomba nieleweke sio kwamba sitaki timu kubadilishwa ama wachezaji mbalimbali kutopewa nafasi kwenye timu ya Manchester United ila mabadiliko ambayo Mou ameendelea kuyafanya yanaonyesha dhahiri kwamba bado kuna mgagaziko wa nani ni nani na katika eneno gani ndani ya United.
Hii ni mifano michache tu ambayo inaweza kukupa picha ya namna ambavyo Mourinho mpaka sasa jambo kubwa linalomsumbua ni kukosa kujua kikosi chake mahiri ni kipi, ni kama kusema Mou mpaka sasa hana “perfect combo” karibu katika eneo la uwanja.
Ukiachana na kelele nyingi kutoka kila pande za ulimwengu kuhusu ubovu wa Paul Pogba na namna ambavyo mpaka sasa hajatimiza matarajio ya wengi huku wengine wakimtaka Mourinho amweke benchi nahodha Wayne Rooney ambaye nae anaonekana kama “anawazingua” mashabiki wa United yote kwa yote ila “MOU KUKOSA KUJUA KIKOSI CHAKE CHA KWANZA ” ndiyo kunaleta matokeo ya maeneo mengine uwanjani kupwaya.
0 comments:
Post a Comment