728x90 AdSpace

  • Latest News

    Tuesday, March 14, 2017

    Simba waipania kanda ya ziwa


    Dar Es Salaam,Tanzania.
    SIMBA imepania kuondoka na pointi zote tisa katika Kanda ya Ziwa ili kujiweka vizuri katika mbio zake za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
    Simba juzi ilishinda Polisi Morogoro kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki, huku Machi 19 inatarajia kucheza dhidi ya Madini ya Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid katika mchezo wa Kombe la Shirikisho.
    Mechi hizo zote zinachukuliwa na Simba kama maandalizi yake kwa ajili ya zile za Ligi Kuu Tanzania Bara Kanda ya Ziwa wakati watakapocheza dhidi ya Kagera Sugar, Mbao FC na Toto Africans.
    Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema kuwa, Simba itacheza na Kagera Sugar Aprili 2 kwenye Uwanja wa Kaitaba katika mchezo wa Ligi Kuu kabla ya kwenda Mwanza kucheza na Mbao na Toto Africans.
    Kocha wa Simba, Joseph Omog ameonesha matumaini ya timu yake kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara mechi zilizobaki na kutwaa taji hilo.
    Alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tisa katika mechi zao za Kanda ya Ziwa watakazocheza kuanzia Aprili 2.
    Simba haijashiriki mashindano ya kimataifa kwa misimu kadhaa, ambapo sasa inapambana katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kuhakikisha inapata nafasi hiyo.
    Mshindi wa kwanza wa Kombe la Shirikisho atapata nafasi ya kuwakilisha taifa katika Kombe la Shirikisho la Afrika. Omog amekuwa na matumaini makubwa na timu yake kufanya vizuri, hasa baada ya baadhi ya wachezaji wake majeruhi kurejea uwanjani baada ya kupona.
    Simba ndiyo wanaoongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 55 wakifuatiawa na mabingwa watetezi Yanga wenye pointi 53 huku Azam FC wakishika nafasi ya nne na pointi zao 44.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Simba waipania kanda ya ziwa Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top