Juma Matandika.
Dar Es Salaam,Tanzania.
MAAFISA wa TFF waliokua wanashutumiwa kuomba rushwa ya shilingi milioni 25 kutoka kwa viongozi wa timu ya Geita Gold Sports ameachiwa huru leo asubuhi baada ya Mahakama ya Kisutu kutupilia mbali ushahidi wa sauti uliowasilishwa mahakamani hapo.
Maafisa hao ni Juma Matandika ambae ni Msaidizi wa Rais wa TFF Jamal Malinzi, na Martin Chacha aliyekuwa mkurugenzi wa mashindano wa TFF.
Wawili hao walifikishwa mahakamani baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwatia hatiani kufuatia madai ya kurekodiwa wakiomba rushwa ya Sh. milioni 25 kutoka kwa viongozi wa Chama Cha Soka Geita (GFA) ili kuisaidia timu yao kupata nafasi ya kupanda Ligi Kuu Tanzania.
Mapema baada ya shutuma hizo, Chacha alijiuzulu nafasi ya Ukurugenzi wa Mashindano TFF, wakati Matandika alisimamishwa kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa kesi hiyo.
Ilidaiwa Februari 4, mwaka jana viongozi hao wa GFA na klabu ya Geita Gold,Salum Kulunge na Constantine Morandi,walikwenda TFF kwa ajili ya kufuatilia rufaa kuhusu uhalali wa usajili wa mchezaji Mohammed Jingo wa timu ya Polisi Tabora,lakini kwa sababu timu ya Geita Gold Mine ilikuwa inachuana na Polisi Tabora kuwania nafasi ya kupanda Ligi Kuu kutoka Kundi C,wakashawishiwa na Maofisa hao wa TFF kutoa rushwa ya Sh. milioni 25.
Ilielezwa washtakiwa waliomba rushwa kuishawishi TFF na Idara ya Uhamiaji Tanzania kutoa uamuzi wa Rufaa dhidi ya Polisi Tabora ili kuisadia Geita kupanda Ligi Kuu. Na baada ya kesi hiyo kuunguruma kwa takriban mwaka mmoja, leo watuhumiwa wote wameachiwa huru.
Matandika anaweza kurejeshwa kazini moja kwa moja baada ya Mahakama kumsafisha,wakati Chacha anaweza kurudi iwapo tu yeye mwenyewe ataamua na TFF itakuwa tayari kumpokea tena.
0 comments:
Post a Comment