Barcelona,Hispania
LIONEL Messi (Pichani) amefunga mabao mawili na kuiwezesha Barcelona kuichapa Valencia mabao 4-2 katika mchezo mkali wa La Liga uliochezwa kwenye dimba la Camp Nou huko Barcelona.
Eliaquim Mangala alianza kuwashtua Barcelona baada ya kuifungia Valencia bao la kuongoza katika dakika ya 29 lakini bao hilo halikudumu sana kwani katika dakika 35,Luis Suárez aliisawazishia Barcelona akitumia vyema mpira uliorushwa haraka na Neymar.
Messi aliifungia Barcelona bao la pili kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 44.Mkwaju huo wa penati ulipatikana baada ya Mangala kumwangua Suarez ndani ya boksi na beki huyo Mfaransa kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Munir El Haddadi aliisawazishia Valencia katika dakika ya 46 na kufanya mchezo uende sare matokeo yakiwa sare ya mabao 2-2.
Kipindi cha pili Barcelona iliielemea Valencia na kushuhudiwa ikipata mabao mengine mawili kupitia kwa Messi katika dakika ya 52 na André Gomes katika dakika ya 89.
Kwa ushindi huo Barcelona imebaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 63 , pointi mbili nyuma ya vinara Real Madrid wenye pointi 65 na mchezo mmoja mkononi.
0 comments:
Post a Comment