Turin,Italia.
JUVENTUS imejiweka katika mazingira mazuri ya kutinga fainali ya michuano ya kombe la Coppa Italia baada ya jana Jumanne usiku kutoka nyuma na kuichapa Napoli mabao 3-1 katika mchezo wa nusu finali ya kwanza uliochezwa huko Juventus Arena.
Napoli ndiyo waliotangulia kupata bao katika dakika ya 38 kupitia kwa Jose Maria Callejon akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Lorenzo Insigne pamoja na Arkadiusz Milik ambao waligongeana vizuri kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.
Paulo Dybala aliisawazishia Juventus bao katika dakika ya 47 kwa mkwaju wa penati baada ya kufanyiwa madhambi ndani ya boksi na Kalidou Koulibaly.
Mfungaji bora wa msimu uliopita Gonzalo Higuain aliifungia Juventus bao la pili katika dakika ya 64 akitumia vyema makosa ya kipa wa Napoli Pepe Reina aliyeshindwa kuicheza vyema krosi ya Juan Cuadrado.
Paulo Dybala kwa mara nyingine aliifungia bao Juventus katika dakika ya 69 kwa mkwaju wa penati uliopatikana baada ya kipa wa Napoli Pepe Reina kumfanyia madhambi Juan Cuadrado.
Timu hizo zitarudiana tena April 5,2017 huko Stadio San Paolo na mshindi wa jumla atafuzu hatua ya fainali ya michuano hiyo mikongwe zaidi Italia.
0 comments:
Post a Comment