728x90 AdSpace

  • Latest News

    Saturday, March 11, 2017

    Mbwana Samatta Tupooze machungu ya Boban , Ngasa


    MBWANA Samatta anaitangaza Tanzania kupitia miguu yake aliyoiacha izungumze kuliko kinywa na kurahisisha maisha ya Genk. Maisha ya Genk yako salama chini ya miguu ya Samatta. Mbwana amezaliwa ili afunge na mashabiki wafurahi. Amezaliwa awe hivi alivyo. Ni ngumu kumtenganisha na nyavu.

    Ndiyo maana kwake ni jambo la kawaida kusikia alifunga jana, akafunga leo. Na rahisi kumbashiria atafunga kesho na atafunga na kesho kutwa. Huyu ndiye Samatta ambaye kuna wakati hubishana na nafsi juu ya Utanzania wake. 

    Wachezaji wa Kitanzania hawako kama alivyo yeye. Wao wako kwa ajili ya kuzitumikia timu kubwa za nyumbani na wakikaribia kuchomwa na jua la Alasiri hujipeleka Mwadui Fc, Mtibwa Sugar, Mbao kumalizia maisha yao.

    Hizi ndiyo akili za wachezaji wetu walioamua kubaki nyumbani wakisubili Samatta aje na  kupiga nae selfie kisha wapost na wengine wamuombe earphone kwa ajili ya kusikilizia muziki. Katika hali hii ya akili za wachezaji wetu ndiyo inayonifanya nisiamini kama Samatta ni Mtanzania mwenzetu. Sisi hatuko kama alivyo, sasa anakuwaje Mtanzania? 

    Ni nadra kumpata mchezaji wa Kitanzania akawa na akili za Samatta ambaye wakati huu simu ya wakala wake Nicholaus Onnise iko bize ikiita simu za matajiri wa vilabu mbalimbali ulaya wanaomtaka mteja wake kwa ajili ya kumsajili. Kila bao analofunga hivi sasa linapandisha thamani yake sokoni. Mpaka kufikia Dirisha kubwa la usajili barani Ulaya Samatta atakuwa miongoni mwa nyota ghali.

    Kaka yangu wa kitaani Abdallah Hussein, mara nyingi nikikutana nae kijiweni na nikianza kumpa taarifa za Samatta tangu ametua Ubelgiji hutumia nguvu kubwa kuniaminisha kuwa Tanzania kumepita wachezaji wengi mahiri. Nakubalia nae na nawaheshimu wachezaji hao, lakini kwa umri nilionao sijaona mchezaji kama Samatta.

    Samatta ni icon ya nchi kwenye mpira. Ni kama ilivyo Diamond Platnumz, Ali Kiba wao ni icon ya nchi kwenye muziki wetu. Muda huu ambao wachezaji wa timu za kawaida nchini wakisubili kupokea ofa za kusajiliwa Simba, Yanga, Azam, Samatta anawaza kuondoka Genk na kusonga mbele zaidi. 

    Tuna wachezaji wanaosubili ofa za kujiunga na timu za nyumbani ili wamalize matatizo yao ya kifamilia yanayowakabili, ni wazi itachukua muda mrefu kumpata Samatta mwingine kando ya Farid Mussa na Thomas Ulimwengu walioamua kuweka pamba masikioni na kumfuata aliko Samatta.

    Ukizungumza na wachezaji wengi wa ndani kila mmoja anasema ana ndoto ya kucheza nje. Hii ni kauli iliyotuama kwenye vinywa vyao, lakini kauli hii haiungani na jinsi mchezaji anayewaza kwenda nje anavyotakiwa kuwa. 

    Wengi wanachelewa kulala. Hawayapati yale masaa 8 ya kila siku ya kuupumzisha mwili. Wanazulula sehemu zote za starehe usiku. Wanakula vyakula ninavyokula mimi. Bado wakiingia uwanjani ni wavivu na wengine kwenye mazoezi ni goi goi kabisa, mchezaji huyu anachezaje ulaya? Kucheza nje kunahitajika maandalizi sio blaaah...blaaah. 

    Niliwahi kumwambia Himid Mao yeye atafuata kwenda ulaya na kufanikiwa, kuliko wachezaji wengi wa ndani kama akiamua kufanya hivyo. Himid yuko fiti muda wote, haijalishi kipindi cha mapumziko au kipindi gani. Ndani ya gari lake anatembea na vifaa vya mazoezi. Bado anaishi katika misingi sahihi ya mchezaji professional.

    Kucheza ulaya si kazi ndogo kama kuitekenya gari funguo na gari ikawaka kisha safari ikaanza. Shekhan Rashid, aliwahi kuniambia hivi. Wachezaji wetu wana mengi yanayowakwamisha kucheza ulaya na wengi hawajazoea kuishi mbali na marafiki zao ndio maana wakienda huko hawachukui muda mrefu wanarudi wakiwa na sababu nyepesi na zile zile za siku zote 

    Kama mchezaji wa Dar es Salaam anashindwa kutulia zake kambini hapo Manungu tu na akili yake ikawaza zaidi huko aliko na sio huku alikotoka, mchezaji huyu anawezaje kuwa na ustahamilivu wa kukaa Kenya na kucheza hata kwa miezi 6? Hawezi kukaa, zaidi atarudi jijini na sababu zile zile. Hawa ndio wachezaji ambao ni marafiki zetu, tunaokaa nao kitaani na kushinda wote maskani. 

    Anapotokeza Samatta na kuwa mchezaji wa tofauti na wenzie ni lazima nimshangae na kupingana na nafsi juu ya Utanzania wake.  Wachezaji wa Kitanzania hawana uvumilivu alionao ndiyo maana ni stori za kawaida tunapokuwa maskani kuanza kudanganyana kuwa ni zari tu limemuangukia Samatta. Unafikaje ulaya na kufikia hatua ya kuwachizisha Wazungu kwa zari la Mentali?

    Samatta hajafika pale aliko kwa zari kama wanavyodhani rafiki zangu. Amefika kutokana na kutembea katika misingi yake anayoiamini ndio maana hivi sasa tunamtaja kama shujaa. Njia rahisi ya kufanikiwa ni kufikiri tofauti na wanavyofikiri wenzako.

    Samatta hakuanza kufikiri tofauti wakati huu alioko Genk, alianza kufikiri tofauti tangu wakati ule alipowagomea Simba kucheza kisa hajatimiziwa mahitaji yake mengine waliyokubaliana awali. Mchezaji wa African Lyon wakati ule anawezaje kuidengulia Simba ya staa Mussa Mgosi na viongozi wenyewe kukuna kichwa na kukaa chini kumsikiliza? 

    Kila zuri la Samatta hivi sasa linafuta machozi tuliyowahi kububujikwa nayo huko nyuma juu ya Haruna Moshi 'Boban' na Mrisho Ngassa. Hawa walitakiwa kuwa mastaa wanaotoka ulaya hivi sasa kuja kuipigania jezi yetu ya timu ya taifa na Samatta angetakiwa kupokewa na kaka zake hao kwenye safari yake ya Ubelgiji na sio yeye kuwapokea Farid na Ulimwengu.

    Lakini haikuwa hivi, badala yake Boban na Ngassa, walituangusha muda ambao tulihitaji kukaa juu ya mabega yao kama ngazi ya kufika waliko jirani zetu Uganda, wao walirudi nyuma hatua 20 na wakikutana na rafikizo walijipongeza na kushindwa kujua ni jinsi gani walivyowaumiza Watanzania. 

    Boban, Ngassa waliwahi kusimama kama alama yetu nchini na kila mmoja akisimama nyuma yao na kuamini wao ndio askari sahihi wa kushika kalamu na karatasi kuchora ramani ya vita. Lakini walichokifanya walikijua wenyewe. Kupanga ni kuchagua. Wamechagua walichokipanga.  

    Wakati huu ambao Samatta anasubiri simu ya Onnise kutakiwa aende kusaini dili la maana, Ngassa ameshaweka wazi mipango yake kuwa kufikia mwishoni mwa msimu huu anaondoka Mbeya City. Boban yeye mara ya mwisho nilimuona uwanja wa Makurumla, Magomeni akipasha na chama langu la kitaa Friends Ranger (Chama la wana/ Ranger chungu).

    Waliotakiwa kumpokea Samatta ulaya na kumfundisha jinsi ya kuishi huko, bahati mbaya waliamua kurudi nyumbani mapema tu na Samatta ameenda huko mwenyewe na amejipokea mwenyewe anaishi mwenyewe, amezoea mwenyewe, lakini kwa kila zuri analofanya hivi sasa ni kutupoza makovu ya vidonda vya kaka zake Boban na Ngassa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Mbwana Samatta Tupooze machungu ya Boban , Ngasa Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top