Dar es salaam,Tanzania.
KINARA wa mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara inayoelekea ukingoni Amissi Tambwe,amesema kutotamba kwake kwenye michuano ya kimataifa ni kutokana na ubora wa timu
shiriki.
Tambwe ambaye ni raia wa Burundi ndiye anayeongoza katika chati ya wafungaji katika Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa amepachika mabao 21 mpaka sasa.
Hata hivyo, mambo yanaonekana kuwa
magumu kwa Tambwe kwa upande wa michuano ya kimataifa ambayo klabu yake ya Yanga ilianza kwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa na Al Ahly ya Misri na sasa Kombe la Shirikisho lakini hajafanikiwa kufunga bao hata moja.
Akizungumza Tambwe alisema mbali na uimara wa timu shiriki katika michuano ya kimataifa, amekuwa akiathiriwa na mfumo wa kocha wake mkuu, Hans Van de Pluijm, ambaye amekuwa akimtumia
kama mshambuliaji wa kati kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini michuano ya kimataifa anamtumia kama winga.
“Lazima tukubaliane kwamba michuano ya kimataifa ni migumu kwani unakutana na timu kutoka mataifa tofauti ndiyo maana nashindwa kufanya yale ninayoyafanya Ligi Kuu,” alisema.
Tambwe alisema atahakikisha anamaliza ukame huo kwenye mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola kwa kuhakikisha anafunga bao.
Yanga itacheza mechi ya marudiano dhidi ya Esperanca nchini Angola ikiwa ni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment