Dar es Salaam,Tanzania.
KUNA kila dalili za Klabu ya Yanga kuondolewa kuwa mwanachama wa
Shirikisho la Soka barani Africa (CAF) endapo itaendelea kukaidi kufanya
uchaguzi mkuu kama ilivyoagizwa na Serikali kupitia Baraza la Michezo
Tanzania (BMT).
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF,
Aloyce Komba, alisema kwamba zoezi la kuchukua fomu kwa wagombea ilikuwa
lianze jana, lakini limeshindikana kutokana na uongozi wa Yanga kukaa
kimya na kuvuruga ratiba yote kama ilivyopangwa.
“Kuna dalili za uongozi wa Yanga kuhujumu uchaguzi huo usifanyike
kwani mpaka sasa wamevuruga ratiba ya uchaguzi huu na tayari tuliwapa
mfano wa fomu za uchaguzi huo ili zitengenezwe na kisha kurejesha TFF,
lakini mpaka (leo) tunaona kimya na hawajasema lolote,” alisema Komba.
Komba ambaye pia ni Mwanasheria alisema kuwa kipindi hiki ambacho
timu ya Yanga inashiriki kwenye mashindano ya kimataifa, ilitakiwa
kufanya uchaguzi kwani wanaweza kufika mbali na moja kati ya timu
ikabaini kwamba wameondolewa na timu ambayo si mwanachama wa CAF
wanaweza kuondolewa.
“Yanga inashiriki mashindano ya CAF na shirikisho hilo likigundua
kwamba viongozi wake hawapo kihalali madarakani na haina leseni ya klabu
inayolitambua, inaweza kuondolewa na kuwa pigo kubwa kwao,” alisema
Komba.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Uchaguzi TFF alisema kuwa shirikisho
hilo limeshaziagiza klabu nchini kukamilisha taratibu za kanuni mpya ya
Leseni za Klabu (Club Licensing) na vijana hao wa Yanga mpaka sasa
hawana leseni ya CAF, hivyo Watanzania wasishangae watakaposikia
imeondolewa kwenye Kombe la Shirikisho.
Komba alisema kuwa mvutano wa uchaguzi unaotaka kufanyika sasa
utapelekea CAF kushtuka na kuja kufanya ukaguzi wa siri kwa lengo la
kubaini kama klabu za hapa nchini zina sifa za kuitwa klabu za Ligi Kuu
bila kuwa na leseni yake.
Aidha, Komba alisema kwamba kamati yake inatarajia kutoa tamko lake
leo juu ya hatima ya uchaguzi huo baada ya uongozi wa Yanga kukaidi
kutekeleza kama Serikali ilivyoagiza.
TFF hivi karibuni ilitangaza uchaguzi mkuu wa Klabu ya Yanga kuwa
ufanyike Juni 25, mwaka huu badala ya Juni 5 iliyokuwa imepangwa hapo
awali. Kwa mujibu wa ratiba ya TFF, fomu za kuwania uongozi wa Yanga
zilitakiwa kuanza kuchukuliwa Mei 25 mwaka huu jambo ambalo limeshindwa
kufanyika.
Serikali iliitaka klabu hiyo kutumia katiba ya mwaka 2010 na kwamba
wanachama wa Yanga watatumia kadi za kawaida za uanachama na si za
benki. Juhudi za kuwapata viongozi wa Yanga kuzungumzia suala hilo
ziligonga mwamba kutokana na simu zao kuita bila kupokelewa.
CHANZO:BINGWA
0 comments:
Post a Comment