Idrissa Traore
Cairo,Misri.
Shirikisho la vyama vya soka Afrika CAF limeiondoa AS Vita ya DR Congo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuikuta na hatia ya kumchezesha mchezaji Idrissa Traore aliyekuwa akitumikia adhabu ya kufungiwa.
Hatua hiyo ya CAF imekuja baada ya kuridhika na rufaa iliyokatwa na Stade Malien ya Mali ikiituhumu AS Vita kumchezesha Traore aliyekuwa nyota wake wa zamani wakati ikijua fika kuwa bado anatumikia adhabu ya kufungiwa.
Kabla ya kutua AS Vita Traore aliichezea Stade Malien msimu wa 2015 ambako alikutana na adhabu ya kufungiwa michezo minne.Baada ya kutua AS Vita Traore alichezeshwa mchezo wa awali dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar mwezi Februari wakati akipaswa kuwa nje kwa michezo mitatu zaidi.
Kwa mujibu wa sheria za CAF timu ya mwisho kucheza na timu itakayoondolewa mashindanoni kwa kukiuka sheria/taratibu ndiyo itakayopewa nafasi ya kuchukua nafasi iliyoachwa wazi.
Hii ina maana kwamba Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyotupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya 16 bora na AS Vita kwa faida ya goli la ugenini ndiyo inayochukua nafasi hiyo na siyo Stade Malien iliyokata rufaa.
0 comments:
Post a Comment