Dar es Salaam,Tanzania.
KOCHA
Mkuu wa muda wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC,
Dennis Kitambi, amesema kuwa udhaifu walioufanya pembeni ya uwanja ndio
umepelekea kupoteza fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports
Federation Cup) dhidi ya Yanga.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB iliweza kupoteza fainali hiyo
jana jioni kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Yanga, bao la matajiri hao wa
Azam Complex likifungwa na Didier Kavumbagu huku Amissi Tambwe akifunga
mawili kwa upande wa Yanga na Deus Kaseka akitupia la tatu.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
mara baada ya mchezo huo Kitambi alisema Yanga wamefanikiwa kutumia
vema mashambulizi yao pembeni ya uwanja na kupata mabao mawili kupitia
eneo hilo.
“Kwa hiyo kutokuwa makini kuzuia mashambulizi yao pembeni ya uwanja
hiyo ndio ilikuwa udhaifu, wakati wa mapumziko tulijitahidi kusema
lazima tutumie njia yoyote ile ya wao kutushambulia kupitia pembeni ya
uwanja, hasa hasa krosi ambazo kipindi cha kwanza zilikuwa zikitupa
matatizo.
“Lakini napenda kuwapongeza wachezaji wangu walifanikiwa kupambana
vizuri hata Yanga walipotangulia kutufunga bao la kwanza dakika ya tisa
hata kipindi cha pili tulipofungwa bao la pili bado waliweza kujibu
mashambulizi, lakini hatukuweza kutengeneza nafasi nyingi za kutosha za
kuweza kushinda mchezo,” alisema.
Kitambi alichukua nafasi hiyo kusema kuwa hakuna wa kualaumiwa baada
ya Azam FC kupoteza fainali hiyo kwani wameshindwa kwa pamoja kama timu
na kudai kuwa kwa sasa wanatakiwa kujipanga zaidi kwa ajili ya msimu
ujao.
Kocha huyo wa zamani wa Ndanda jana alisaidiana majukumu ya benchi la
ufundi pamoja na Kocha Msaidizi wa Vijana wa timu hiyo, Idd Cheche,
ikiwa ni mechi yao ya pili kusimamia benchi hilo baada ya ile ya kufunga
pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mgambo JKT
iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.
Wawili hao wameshika majukumu hayo baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa
Azam FC Stewart Hall kuachia ngazi akitaka kwenda kupata changamoto
nyingine ya ufundishaji nje ya Tanzania.
Tayari uongozi wa Azam FC umeshaziba nafasi yake kwa kuingia mkataba
na makocha kutoka nchini Hispania, Zeben Hernandez (Kocha Mkuu), Jonas
Garcia (Kocha wa Viungo), huku wengine wakitarajia kuongezeka Julai
mwaka huu katika eneo la Kocha wa Makipa, Kocha Msaidizi atakayesaidiana
na Kitambi pamoja Daktari wa timu.
0 comments:
Post a Comment