Dar es Salaam,Tanzania.
Fainali za Kombe la Shirikisho maarufu kama Azam Sports Federation
Cup (ASFC) zinatarajiwa kufanyika kesho Mei 25, 2016 kwa kuzikutanisha
timu za Young Africans na Azam FC; zote za Dar es Salaam katika mchezo
utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini.
Sherehe za mchezo huo zitaanza rasmi saa 8.00 mchana kwa mchezo wa
awali wa kuburudisha kuzikutanisha timu za soka za kituo cha Televisheni
cha Azam ‘Azam Tv’ na wafanyakazi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
na kurushwa live na kituo hicho kilichotokea watazamaji wa nchi za
Afrika Mashariki na Kati.
Viingilio katika mchezo huo itakuwa ni Sh 25,000 kwa VIP A wakati VIP
B na C ni Sh 20,000 wakati majukwaa yenye viti vya rangi ya chungwa,
mzunguko wenye viti vya rangi ya bluu na kijani ni Sh 5,000.
TFF inajivunia nyota wake kama Jemedari Said, Wilfred Kidao, Salum
Madadi, Alfred Lucas, Danny Msangi, Michael Ngogo na Jonas Kiwia, lakini
Meneja wa timu ya Wafanyakazi wa TFF, Eliud Mvella anasikitika kumkosa
nyota wake Mwesigwa Selestine.
Azam Tv wanatamba na nyota wao waliopata kufanya kazi nje ya nchi
katika vyombo vya kimataifa kama vile Charles Hilary, Tido Mhando,
Yahaya Mohammed, Baruan Muhuza na Rhys aliyetajwa kwa jina moja.
Mbali ya burudani hiyo, pia Mwakilishi wa Azam Tv, Baruan Muhuza
alisema kwamba mara baada ya mchezo huo utakaomalizika saa 9.00 alasiri,
itafuata burudani ya wasanii mbalimbali ambao pia wataburudisha wakati
wa mapumziko ya mchezo huo.
Alisema kwamba burudani hiyo itakuwa ni ya nusu saa kabla ya kuziacha
timu kufanya maozezi ya kupasha moto viungo kabla ya mchezo huo kuanza
saa 10.30 jioni na wakati wa mapumziko burudani itaendelea kabla ya
kutolewa taji ambalo timu zitakuwa zikiliwania.
Kwa mujibu wa kanuni bingwa wa michuano hiyo atatwaa kombe, medali na
fedha Sh 50,000,000 wakati mshindi wa pili atazawadiwa tuzo na medali.
Kadhalika kutakuwa na tuzo kwa mchezaji bora, mfungaji bora na mchezaji
bora wa michuano hiyo ambayo waaandaaji wamepanga kuiboresha mwakani.
Mwamuzi wa mchezo huo atakuwa Israel Mujuni Nkongo wa Dar es Salaam
kwa mujibu wa Kamati ya Waamuzi ya TFF huku akisaidiwa na Ferdinand
Chancha wa Mwanza upande wa kulia (line 1) na upande wa pili ni Soud
Lila wa Dar es Salaam (line 2) na mwamuzi wa akiba mezani ni Frank Komba
wa Dar es Salaam pia. Kamishna wa mchezo huo anatakuwa Juma Mgunda wa
Tanga.
Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu msimu 2015/16, mabingwa wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara msimu 2015/16 wataiwakilisha nchi katika
michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2016/17. Nafasi hiyo
imechukuliwa na Young Africans.
Kadhalika Azam ina tiketi tayari ya kushiriki Kombe la Shirikisho
Barani Afrika kwa kufika fainali za ASFC ingawa kanuni zinataka bingwa
ambako kwa upande wa Yanga wana tiketi ya michuano ya juu zaidi ya
shirikisho. Mvuto wa mchezo wa Jumatano ni ushindani wa soka na zawadi
kwa bingwa.
Fainali za Kombe la Shirikisho zinakuja baada ya mchuano
ulioshindanisha timu 64 za Ligi Kuu Tanzania Bara - VPL (16); Ligi
Daraja la Kwanza -FDL (24), Ligi Daraja la Pili – SDL (24).
0 comments:
Post a Comment