Dar es Salaam,Tanzania.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda anayeichezea Simba ya Dar
es Salaam, Hamisi Kiiza, amewataka viongozi wa timu hiyo kuwa na shukrani kwa kazi aliyowafanyia hadi kumaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu
uliomalizika hivi karibuni.
Kiiza ndiye mfungaji bora wa Simba akifunga mabao 19, akizidiwa mawili na mshambuliaji wa Yanga Amissi Tambwe.
Kiiza anayetajwa kuwa ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni anayetarajiwa kutupiwa virago kutokana na kuonesha nidhamu mbovu, alisema yupo tayari
kuachana na timu hiyo kwa sababu Simba wamekosa shukrani, licha ya mchango mkubwa alioutoa.
“Nipo tayari kuachana nao, ingawa najivunia kiwango bora nilichokionesha hata kumaliza nafasi ya pili kwa ufungaji, isipokuwa uongozi wa Simba hauna shukrani kwa sababu kudai haki yangu ndiyo ilikuwa sababu ya kuonekana sina nidhamu,” alisema Kiiza.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kuichezea Yanga pia kwa mafanikio,alisema uwezo aliouonesha akiwa na Simba msimu huu, anaamini hawezi kukosa timu ya kuchezea. Alisema aliamua kurudi Tanzania kutokana na ushindani uliopo kwenye ligi na pia maslahi mazuri tofauti na Uganda, lakini pamoja na yote hawezi kukataa kucheza kwao kwa sababu ndiko alipoanzia.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Simba,Evance Aveva alitaja sababu mbalimbali zilizofanya Simba ising’are mwaka huu mojawapo ikiwa ni utovu wa nidhamu wa baadhi ya wachezaji ambao walifikia hadi kugoma.
0 comments:
Post a Comment