Manchester, England.
Timu ya Taifa ya England imeanza vyema maandalizi ya kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa michuano ya Ulaya hapo mwezi Juni baada ya usiku huu kuichapa Timu ya Taifa ya Uturuki kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa katika uwanja wa Etihad jijini Manchester.
Wenyeji England ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 2 tu ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wake Harry Kane lakini wageni Uturuki walikuja juu na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 13 kupitia kwa kiungo wake Hakan Calhanoglu na kufanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili wenyeji England wakichagizwa na mashabiki wao waliipa wakati mgumu Uturuki na kufanikiwa kupata penati ambayo haikuzaa matunda baada ya mpigaji Harry Kane kukosa.Penati hiyo ilitolewa baada ya Jamie Vardy kuangushwa kwenye eneo la hatari na mlinzi wa Uturuki Topal.
Katika dakika ya 83 mchezo ukiwa unaelekea ukingoni Jamie Vardy aliuwahi mpira uliokuwa unazagaa langoni kwa Uturuki na kufunga kwa shuti la karibu na kuiandikia England bao la pili na kufanya mchezo uishe kwa wenyeji kutoka uwanja kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-1
0 comments:
Post a Comment