Waamuzi watatu wa soka kutoka Uganda, ndio wakaochezesha mchezo wa
kirafiki wa kimataifa kati ya Taifa Stars ya Tanzania na Harambee Stars
ya Kenya utakaofanyika Uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi, Kenya.
Waamuzi hao watakaochezesha mchezo huo utakaoanza saa 10.00 jioni na
kurushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Azam Tv kwa
kushirikishi na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) ni Brian Nsubuga
atakayepuliza kipenga na wasaidizi wake ni Bugembe Hussein upande wa
kulia (line 1) na Katenya Ronald kwa upande wa kushoto (line 2).
Kamishna wa mchezo atakuwa Amir Hassan kutoka Somalia ambako Meneja
wa Uwanja wa Moi Kasarani, Lilian Nzile amesema kwamba mazingira uwanja
ni mazuri na mipango yote ya mchezo huo imekaa vema ikiwa ni pamoja na
usalama uliothibitishwa pia na Kanali wa Jeshi la Polisi, Muchemi Kiruhi
OCS wa Kasarani.
Kwa upande wa Kocha Mkuu Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya
Kilimanjaro inayozalishwa na Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL), Charles
Boniface Mkwasa atawakosa washambuliaji wake watatu katika kikosi
ambacho kitaivaa Harambee Stars.
Washambuliaji hao ni Mbwana Samatta kutoka Genk ya Ubelgiji, Thomas
Ulimwengu anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC)
na John Bocco ambaye ni majeruhi wa mguu aliumia wakati wa fainali za
Kombe la FA kati ya Yanga na Azam Jumatano wiki hii.
“Madaktari wamempa Bocco saa 72 za mapumziko. Bila shaka kabla ya
kucheza na Misri atakuwa amepona,” alisema Mkwasa leo Mei 28, 2016
asubuhi na kuongeza kuwa Samatta ametuma taarifa kukosa mchezo dhidi ya
Kenya kwa kuwa ana ratiba ya kucheza mchezo muhimu Mei 30, mwaka huu na
matarajio ni kujiunga na timu Juni 1, 2016 kabla ya kuivaa Misri Juni 4,
mwaka huu.
Kwa upande wa Ulimwengu, uongozi wa TP Mazembe nao waliomba kumtumia
Ulimwengu katika mchezo wa ushindani wa mpinzani wake AS Vita. TP
Mazembe na AS Vita ni timu pinzani huko DRC Congo na uongozi wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ukaridhia na Mkwasa sasa amejipanga
kukiandaa kikosi bila nyota hao mahiri.
“Katika mchezo huu sitakuwa na professionals (wachezaji wa kulipwa),”
alisema Mkwasa ambaye jioni ya leo ameahidi kutoa kikosi cha nyota 11
watakaonza dhidi ya Kenya kesho.
Kwa sasa anaangalia namna ya kuipanga vema safu yake ya ulinzi baada
ya kumkosa Kelvin Yondani anayetumikia adhabu ya kuonywa mara mbili kwa
kadi ya njano hivyo kutojumuishwa kwenye mipango mchezo dhidi ya Misri.
Mabeki anaotarajiwa kuanza nao ni Juma Abdul upande wa kulia na Mohammed
Hussein upande wa kushoto.
Walinzi wakaoachukua nafasi ya Yondani na Nadir Haroub Cannavaro
ambaye hakuongozana na timu katika safari ya Kenya ni Erasto Nyoni,
Aggrey Morris na David Mwantika huku viungo wa kati wanaotarajiwa
kupangwa ni Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude na pembeni ni Farid Mussa na
Shiza Kichuya. Washambuliaji watakaotikisa Kenya katika mchezo wa kesho
ni Elisu Maguli na Ibrahim Ajib.
“Kipa anaweza kuanza Dida (Deo Munishi) au Aishi Manula. Lakini hao
niliokutajia ni proposed team (kikosi tarajiwa), lakini hasa nani anaaza
kesho nitakutajia jioni ya leo mara baada ya mazoezi pale Moi
Kasarani,” alisema Mkwasa aliyeonekana kujiamini na mipango yake kama
lilivyo jina lake la umaarufu la Master.
“Nimeiandaa timu kucheza mifumo miwili ambayo ni 4-3-3 ambao ni mfumo
wa kushambuliaji na pale tutakapokuwa tuna-defense (tunazuia) basi
mfumo utakuwa ni 4-5-1,” alisema Mkwasa.
Katika mchezo wa kesho Mkwasa anayesaidia na Hemed Morocco na Manyika
Peter anayewanoa makipa atapata nafasi ya kubadili wachezaji hadi sita
ambao ni utaratibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa mechi
za kirafiki za kimataifa kadhalika makubaliano katika mkutano wa kabla
ya mchezo wa kesho.
Stars iliwasili Nairobi, Kenya jana asubuhi na kupokewa na wenyeji
Shirikisho la Soka Kenya iliyowapeleka hoteli ya Nairobi Safari Club
iliyoko mtaa wa Koinange, katikati ya jiji la Nairobi ambako mchana
kabla ya kwenda mazoezi ilitembelewa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya,
Dk. John Haule aliyewahakikishia usalama timu hiyo licha ya kuwako kwa
taarifa za kuvamiwa.
“Msaada wowote mnaotaka na chochote mnachohitaji tunaomba mtutaarifu
tujue namna ya kuwasaidia. Msiwe na wasiwasi kabisa. Hata kama
hamjaipenda hoteli, semeni,” alisema Dk. Haule ambaye aliitakia timu
mafanikio mazuri katika mchezo wa dhidi ya Harambee na ule wa Mafarao wa
Misri.
Viongozi wa msafara wa Taifa Stars, Ahmed Mgoyi na Omar Walii
walimweleza Balozi DK. Haule kuridhika na kambi na kwamba hawakupata
tatizo lolote hali ilivyo hadi sasa.
0 comments:
Post a Comment