NAIROBI,KENYA
Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Charles Boniface Mkwasa
amesema kwamba mchezo ujao kati ya Mapharao wa Misri na Taifa Stars,
utakuwa ni fainali ya kuamua taifa litakalofuzu katika fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika AFCON hapo mwakani kutoka kundi G.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo kati ya
Harambee Stars ya Kenya na Taifa Stars ya Tanzania Mei 29, 2016,
uliofanyika Uwanja wa Moi Kasarani, Mkwasa maarufu kama Master anasema
kwa msimamo na hali ilivyo kwa sasa, “Najua Misri wanatufuatilia. Na
hata Kenya kwa siku zote tatu walikuwako. Najua Misri wanahitaji sare
ili wafuzu kwa fainali hizi, lakini hawataipata Tanzania.”
Mkwasa anasema mchezo dhidi ya Misri, ana uhakika vijana wake
watajitahidi ili kupata matokeo mazuri baada ya Jumapili kufanya vema
dhidi ya Harambee Stars waliocheza mechi hiyo mbele ya mashabiki wao
wachache ambao pia hawakuchangamka kama wale wa Tanzania ambao licha ya
kuwa ugenini walichangamsha mji na uwanja.
Wakati Misri wana pointi saba, Taifa Stars ina pointi moja na hivyo
wa kuibania au kupindua matokeo ya Misri isiende AFCON mwakani, basi ni
Tanzania hasa kama itawafunga Mapharao Jumamosi kabla ya kwenda Nigeria
Septemba, mwaka huu kucheza na Nigeria.
“Kama nilivyosema, Misri wanakujawanahitaji pointi moja. Lakini sisi
tunahitaji pointi tatu. Mchezo wa leo unatosha kuona mapungufu
(upungufu). Maana ilikuwa mechi ngumu iliuyojaa nyota wote wa Kenya
ambao ni professionals, lakini mimi nilikuwa na local based players na
matokeo yamekuwa hayo.
“Tilianza kufunga bao, lakini wakarudisha. Bora mchezo umeishia hivi
maana najua Wakenya hawana uvumilivu, tungewafunga hapa sijui kama
tungetoka salama,” amesema Mkwasa ambaye baadhi ya waandishi, hususani
wale wa Kenya walianguka kicheko kuashiria kuwa kuna matatizo katika
utawala wa soka.
Mkwasa anasema ana taarifa namna ambavyo Misri wanaifuatilia Taifa
Star hususani ukusanyaji wa video kwa ajili ya kuona aina ya soka la
Tanzania, huku akisema: “Hawatafanikiwa kwa sababu soccer is the game of
different approach (Soka ni mchezo wenye mifumo tofauti). Hivyo
tulivyocheza na Kenya sivyo nitakavyocheza na Misri, nitakuwa na
approach yake.”
Anasema ushindi wa Jumamosi ijayo ni wa kuvuna pointi tatu ili kupata
kasi ya kushinda mchezo dhidi ya Nigeria na kufungua ukurasa mpya wa
Taifa Stars kutengeneza mazingira mazuri ya kuwashinda Nigeria katika
mchezo wa mwisho hatua ya makundi utakaofanyika Septemba, mwaka huu.
“Tunaomba Wakenya mtuombee. Nasi tunawaombea ili kama wote inatokea
mwaka huu tunakosa mafasi, basi iwe kheri kwa kipindi kijacho. Sisi
tumekuja kucheza kwenu katika mji wenu wenye baridi basi nanyi karibuni
siku moja dar es Salaam, Tanzania katika mji wetu wetu wenye joto,
huenda mkaambulia sare vile vile,” anasema.
Mkwasa alipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (FKF), kwa kuandaa
mchezo huo angalau kwa asilimia 70 kwa kushirikiana na Tanzania
iliyojazia gharama za juu sambamba vijana wake kwa kucheza kwa kujituma
licha ya kuwakosa nyota wake wa kulipwa na hivyo kupata picha na mbinu
sahihi za kuivaa Misri Jumamosi ijayo.
“Bado tunaendele kujenga timu yetu, wengi ni vijana kama mlivyoona na
wengine ni mara ya kwanza wanacheza. Nimewapa nafasi na mmeona uwezo
wao, bila shaka tutafanya vema maana wengine ni under 21 wako kwenye
kikosi. Huko mbele tutakuwa na timu nzuri,” anasema Mkwasa akimtolea
mfano Shiza Ramadhani ambaye alipewa nafasi kwa mara ya kanza katika
kikosi cha kwanza akichukua winga ya kulia.
VICTOR WANYAMA
“Kwa hiyo tayari tumeona kitu gani cha kuongeza,” anasema Mkwasa hoja
yake iliyoungwa mkono na Nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama
ambaye kwa dakika chache, alizungumza na Ofisa Habari na Mawasiliano wa
Shirikisho la Soka Tanzania na kuhoji: “Unasema leo hamkuwa na
professional pale uwanjani?” alipohakikishiwa ukweli huo, akasema:
“Basi mna kikosi kizuri. Wengi ni vijana, wanaweza kama mkicheza kwa
kutubana kama mlivyobana hapa, Misri mnaifunga na hata hao Nigeria, si
ajabu nikasikia mnakwenda AFCON mwakani. Ninaitakia kila la khetri timu
hii, nawatakiwa kila la kheri Watanzania katika harakati zao. Sisi mwaka
huu tumepotea kabisa, hatuna matumaini tena, tunajipanga ndiyo maana
nimekuja kutetea taifa langu, hata kama tumekosa nafasi,” alisema
Wanyama anayekipiga Southampton ya England.
Katika mchezo huo, Taifa Stars iliwakosa nyota wake Mbwana Samatta
anayechezea Genk ya Ubelgiji kwa kuwa alikuwa na mchezo muhimu wa kupa
nafasi timu yake ama icheze Ligi ya Uropa au ibaki nje katika michezo ya
kimataifa ngazi ya klabu Ulaya. Shirikisho la Soka Tanzania na Kocha
Mkwasa walimruhusu kama ilivyo kwa Thomas Ulimwengu anayekipiga TP
Mazembe waliokuwa na mchezo mkali dhidi ya AS Vita ambao wana utani na
ushindani mkali wa soka huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
MWINYI KAZI MOTO
Naye Nahodha wa Taifa Stars katika mchezo huo, Mwinyi Kazimoto
amesema kwamba mchezo dhidi ya Kenya, umeonesha picha ya kinachotakiwa
kufanyika katika michezo ijayo inayoikabili timu hiyo baada ya kusifu
maandalizi, mapokezi mazuri na sapoti nzuri kutoka kwa mashabiki wa
Kitanzania, hasa wale waliosafiri umbali mrefu kutoka Dar es Salaam
kwenda Nairobi, Kenya kuishangilia Stars. Nahodha wa Taifa Stars ni
Mbwana Samatta anayesaidiwa na John Bocco ambao katika mchezo huo,
hawakucheza. Bocco ni Majeruhi.
MCHEZO WA HARAMBEE STARS, TAIFA STARS
Katika mchezo huo, kipindi cha kwanza mashabiki walishuhudia mabao
1-1 kwa kila upande na ndiyo yaliyokuwa matokeo ya mwisho katika dakika
90, lakini kipindi cha pili wadau wa soka walishuhudia mabadiliko ya
kila timu kujaribu nyota wake kwa mujibu wa sheria na taratibu za
Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA), linaloruhusu kubadili wachezaji
hadi wachezaji sita. Lakini hakukuwa na mabadiliko ya matokeo.
Kuhusu mabao ni Elias Maguli ndiye aliyetangulia kuifungia Taifa
Stars bao katika dakika ya 30 kwa kichwa baada ya kupokea krosi murua
kutoka kwa Juma Abdul kutoka Mashariki ya Uwanja wa Moi Kasarani kabla
ya dakika saba baadaye kumfanyia madhambi Winga Ayub Masika ndani ya
eneo la hatari hivyo Mwamuzi, Brian Nsubuga kutoka Uganda, kuamuru
penalti iliyokwamishwa wavuni na Victor Wanyama.
Katika mchezo huo ambao wakati wote ulikuwa ni wa kushambuliana kwa
timu zote mbili, Taifa Stars iliwapumzisha kipa Deogratius Munishi na
nafasi yake ikachukuliwa na Aishi Manula na kwa wakati mmoja kuwatoa
Jonas Mkude na Shiza Ramadhani na nafasi zao kuchukuliwa na Farid Mussa
na Mohammed Ibrahim baadaye Kocha Mkwasa alimwingiza Jeremiah Juma
kuchukua nafasi ya Maguli.
Kenya wao waliwatoa Humphrey Ochieng kwa kuingia Cliford Miheso;
akatolewa tena Jesse Were kwa Wyclif Ochomo; Ayub Masika akapumzishwa na
John Makwata akapewa nafasi kama alivyopumzishwa Anthony Agay na nafasi
yake kuchukuliwa na Mayeko Mohammed. Pamoja na mabadiliko hayo, matokeo
yalibaki vilevile 1-1 hadi dakika ya 90 katika mchezo ambao Wanyama
alipewa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Kazimoto.
VIKOSI VYA TIMU ZOTE
Vikosi vya kwanza katika mchezo, Kenya: 1. Boniface Oluoch, 9.
Joakins Otieno Atudo, 5. Abud Omar Khamis, 12. Eugene Ambuchi Asike, 8.
David Owino Odhiambo, 14. Anthony Akumu Agay, 15. Victor Mugubi Wanyama,
23. Ayub Timbe Masika, 19. Humphrey Mieno Ochieng’ 16. Eric Johanna
Omondi, 29. Jesse Jackson Were
Wachezaji wa akiba: 3. David Okello Abongo, 10. Eric Ouma Otieno, 6.
Mayeko Musa Mohammed, 24. Victor Ali Abondo, 27, Wycliff Okello Ochomo,
20. John Mark Makwata, 21. Clifford Miheso Ayisi
Tanzania XI: 1. Deo Munishi, 6. Juma Abdul Jafari, 2. Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’, 13. Aggrey Morris, 15. Erasto Edward Nyoni, 17.
Jonas Gellard Mkude, 7. Himid Mao Mkami, 16. Shiza Ramadhan Yahya, 12.
Mwinyi Kazimoto Mwitula, 10. Elias Mrugao Maguli, 4. Deus David Kaseke
Wachezaji wa akiba walikuwa: 18. Aishi Salum Manula, 5. David John
Mwantika, 9. Farid Mussa Shah, 11. Jeremiah Juma Ally, 8. Abrahim Hajibu
Migomba, 3. Mwinyi Haji Mngwali, 14. Mohammed Ally Ibrahim
WAAMUZI
Brian Nsubuga
(Mwamuzi wa kati), Hussein Bugembe (Msaidizi wa Kwanza), Ronald Katenya
(Msaidizi wa Pili), Amir Abdi Hassan (Kamishna wa mchezo) and Davies
Omweno (Mwamuzi wa Akiba, Mezani.)
0 comments:
Post a Comment