Siku chache baada ya Yanga kutolewa katika michuano ya Kombe la Kagame, kiungo mkabaji wa timu hiyo, Saidi Juma Makapu, amesema amehuzunishwa na taarifa za watu kusema safu ya kiungo mkabaji ndiyo iliyokuwa tatizo katika kikosi hicho, badala yake amesisitiza Yanga ilitolewa kama timu na si tatizo la mtu mmoja.
Licha ya Yanga kupewa nafasi kubwa ya kufika fainali, iliondolewa hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na Azam kwa mikwaju ya penalti 5-3, huku beki wa timu hiyo, Haji Mwinyi Mngwali akipoteza mkwaju wake.
Makapu hakucheza michuano hiyo kutokana na majeraha.
“Nimeumia sana kusema kwamba kiungo cha Yanga kilipwaya katika Kagame, sisi tunacheza kama timu na siyo mtu mmoja. Kwangu namuona Mbuyu Twite kama mtu aliyekuwa akicheza kwa juhudi uwanjani. Angalia ile mechi na Wasudani (Al Khartoum), alicheza vizuri sana.
“Cha muhimu ni kuchukua hilo kama funzo kwa ajili ya kujiandaa na ligi na michuano ya kimataifa. Naamini urejeo wangu na kwa kushirikiana na wenzangu, utakuwa na faida katika timu yetu,” alisema Makapu.
0 comments:
Post a Comment