Siku moja kabla ya Yanga kuiva Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii, uongozi wa Yanga umefanya tukio ambalo ni kama unataka kurejesha hamasa ya ushindi ambapo umemwaga fedha za usajili ambazo walikuwa bado wanadaiwa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo.
Yanga itakipiga na Azam, kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taif jijini Dar es Salaam ambapo ni lazima timu moja ishinde ikiwa ni ishara ya kufungua Ligi Kuu Bara 2015/16.
Awali, wachezaji hao kabla ya kulipwa fedha hizo, walipanga kucheza chini ya kiwango kwenye mchezo huo baada ya kuona wachezaji wenzao wa kigeni wamelipwa stahiki zao akiwemo beki wa kati raia wa Togo, Vincent Bossou na Mzimbabwe, Thabani Kamusoko ‘Rasta’.
Baadhi ya wachezaji waliokuwa wanadai ni; Salum Telela, Simo Msuva, Kelvin Yondani, Ally Mustapha ‘Barthez’, Deogratius Munishi ‘Dida’, Pato Ngonyani, Juma Abdul na Said Makapu.
Chanzo cha habari kutoka Yanga kimeeleza kuwa, mabosi wa timu hiyo waliamua kukamilisha mali hayo juzi Jumatano kwa kusaini hundi ya malipo ili kuondoa mgawanyiko uliokuwa unaelekea kutokea.
“Uongozi umekamilisha malipo ya wachezaji wetu 13 waliokuwa wanadai fedha za usajili za msimu huu ambazo tulikuwa hatujawakamilishia.
“Hiyo yote imefanyika kurejesha morali kuelekea mechi yetu dhidi ya Azam, ninaamini hakutakuwa visingizio na lawama kwa wachezaji wetu na kama kufungw tufungwe kimchezo na siyo kisingizio cha kutowamalizia fedha zao za usajili,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha kuzungumzia suala hilo, simu y iliita bila kupokelewa.
0 comments:
Post a Comment