KOCHA wa Simba, Dylan Kerr amesema straika wa timu hiyo, Hamis Kiiza amepoteza kujiamini baada ya kushindwa kufunga bao lolote katika mechi nne za kirafiki zilizopita, lakini ana imani kuwa kiwango chake kitarejea endapo atafanikiwa kufunga katika siku za karibuni.
Kwa mara ya mwisho Kiiza alifunga siku Simba ilipocheza na Taifa Jang’ombe visiwani Zanzibar, lakini katika michezo dhidi ya KMKM na kisha mechi tatu za kirafiki jijini Dar es Salaam dhidi ya SC Villa na URA za Uganda pamoja na ile ya Mwadui hakufanikiwa kufunga.
Kerr alisema Kiiza anaweza kuwa na msaada katika timu yake endapo atajitahidi kurejesha hali ya kujiamini na hilo litakuwa jepesi zaidi kama atafunga mabao siku za hivi karibuni.
Kocha huyo alisema kwa kuwa Kiiza amepoteza kujiamini, anakuwa akitaka kulazimisha kufunga hata katika nafasi ngumu badala ya kusubiri timu yake itengeneze nafasi nzuri zaidi za mabao.
“Kiiza amepoteza tu kujiamini kwa sasa, unajua straika anapokaa muda bila kufunga hali ya kujiamini inapungua, anashindwa kufanya kile anachotakiwa kufanya na kutaka kufunga kwa nguvu.
“Straika anaposhindwa kujiamini anakuwa kama mcheza gofu asiyejiamini maana hushindwa kutumbukiza mipira mingi, hivi ndivyo ilivyo kwa Kiiza anatamani sana kufunga lakini haamini kama anaweza kufanya hivyo,” alisema Kerr.
Kwa upande mwingine kocha huyo amewananga wachezaji wake kwa kushindwa kucheza aina ya soka analowafundisha na mara nyingi kucheza kwa namna wanavyofahamu wao wenyewe.
“Kuna wakati wachezaji wangu wananikera sana, wanacheza mpira wao ambao sijui wameutoa wapi, wanakuwa hawachezi kwa namna nilivyowafundisha na hiyo ndiyo sababu unaona timu wakati mwingine inacheza ovyo. Kuna wakati wanatulia na kucheza kwa namna nilivyowafundisha, hapa ndipo unapoiona timu inacheza soka la kuvutia,” alisema Kerr
Mgosi awaapia Simba
Mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amewaapia mashabiki wa timu hiyo kwamba watafunga sana msimu ukianza na si kweli kwamba fowadi yao ni kazi bure. Mgosi amesema hayo kwa kile kinachoelezwa kuwa, wanapata nafasi nyingi lakini hawafungi, kauli ambayo anaamini haina mashiko kwake.
“Nakataa kuwa safu yetu ya ushambuliaji haijui kufunga. Unapozungumzia washambuliaji wanaofunga mabao kwa wingi ni Simba, tatizo lililopo sasa tunakosa umakini na wachezaji hatujazoeana,” alisema.
0 comments:
Post a Comment