Leo katika uwanja wa taifa kutakuwa na mchezo mkali wa ngao ya jamii kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara.
Mchezo huu utazikutanisha Yanga na Azam.Yanga inaingia katika mchezo wa huo ikiwa kama bingwa wa ligi iliyoisha huku Azam wakiingia kama washindi wa pili.Mchezo wa leo ndiyo utakaotupa taswira ya jinsi ligi yetu itakavyokuwa.Mchezo huu umebeba dhamana kubwa sana hasa ukizingatia kuwa vilabu hivi ndivyo vitakavyoiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.
Naufahamu upinzani uliopo kati ya vilabu hivi viwili na ndiyo maana nachukua nafasi hii kutoa rai yangu kwa vilabu hivi kuheshimu viingilio vyetu.Yanga na Azam vinapaswa kutambua kuwa tunahitaji kukata kiu yetu kwa soka la kitabuni.Soka lililokwenda shule.Soka lisilo la kukamiana.Soka la kistaarabu lisilo na ubabe usio na tija kwa vilabu husika na taifa kwa ujumla.
Yanga na Azam zinapaswa kuingia katika mchezo wa leo zikifahamu kuwa macho na masikio ya kila mpenda soka wa nchi hii yatakuwa yameelekezwa uwanja wa taifa.Hivyo zinapaswa kuonyesha tofauti kubwa kiuchezaji,kimbinu na kadhalika.Zinapaswa kuwa ni kioo cha kujitazamia kwa vilabu ambavyo vinautazama mchezo wa leo kama sehemu ya kujitathimini kabla ya kuanza kwa mikikimikiki ya ligi kuu.
Wachezaji wanaswa kufahamu kuwa kitendo chochote kile kisicho cha kiungwana siyo kwamba kitawagharimu wao moja kwa moja bali pia kitaharibu mipango mizima ya timu.Kitaharibu radha ya mchezo.Kitaharibu mbinu za mwalimu na pia kitashusha ari na morali ya mashabiki watakaokuwa uwanjani na wale watakaokuwa wakiufuatilia mpambano huo kupitia redio na televisheni.
Kwa kuhitimisha napenda kuvitakia vilabu vya Yanga na Azam mchezo mwema huku nikivikumbuka kuwa matokeo yoyote yale yatakayopatikana leo ni sehemu tu ya mchezo wala yasiwe chanzo cha kuanza kutimua wachezaji.
0 comments:
Post a Comment