Dar es salaam,Tanzania.
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba, wametaja sababu tano za kuibuka kidedea kwenye mchezo wao wa leo Jumapili dhidi ya Azam utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Simba sasa wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Barawakiwa na pointi 57, huku Azam wakiwa nafasi ya pili baada ya kujikusanyia pointi 58, huku Yanga waliopo kileleni wakiwa na pointi 65.
SOKA EXTRA imekusanya sababu tano ambazo Simba watazitumia ili kuibuka kidedea kwenye mchezo wa leo.
1. Kutolewa FA
Sababu ya kwanza iliyotajwa na Wekundu wa Msimbazi hao kwamba lazima watoke uwanjani na ushindi leo ni kutolewa kwao kwenye michuano ya Kombe la FA hivyo kuamua kuelekeza hasira zao zote kwenye ligi na zaidi ikiwa ni mechi dhidi ya Wanalambalamba hao.
Simba ilitolewa na Coastal Union kwenye mchezo wa robo fainali ambapo kwa sasa nguvu pekee ya wekundu hao wa Msimbazi imebaki kwenye ligi pekee.
2. Ukame wa makombe
Simba kwa miaka mitatu sasa hawajapata kombe la aina yoyote baada ya kujikuta wakimaliza kwenye nafasi ya tatu mpaka ya nne kwenye michuano ya ligi kuu na kuwafanya wapinzani wao Yanga na Azam wapokezane kwenye michuano ya kimataifa.
3. Kushiriki michuano ya kimataifa.
Mara ya mwisho Simba kushiriki michuano ya kimataifa ilikuwa ni mwaka 2012 ilipocheza Klabu Bingwa ya Afrika na kutolewa katika hatua muhimu naWaarabu wa Al Shandy kutoka Sudan hivyo wanataka kushinda mchezo huo ili kurudisha matumaini ya ubingwa na baadaye kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi.
4. Kukata ngebe za wapinzani wao.
Simba wamekuwa wakipata kejeli nyingi
kutoka kwa mashabiki mbalimbali wa soka hapa nchini ambao kwa sasa wamepachikwa jina la ‘wa mchangani’ neno ambalo likitumika kama kuikejeli klabu ambayo kwa miaka mitatu sasa haijashiriki michuano ya kimataifa.Neno hilo limekuwa kero sana kwa mashabiki wa Simba kila wanapolisikia kutoka kwa
watani wao ama timu nyingine yoyote pamoja na ukweli kuwa linafikisha ujumbe sahihi lakini unaoumiza.
5. Kutuliza hali ya hewa Msimbazi.
Hali ya mambo ndani ya Simba kwa sasa si mazuri baada ya mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na imani na viongozi, benchi la ufundi na hata wachezaji baada ya kikosi hicho kupoteza michezo yake miwili ya ligi pamoja na kutolewa kwenye Kombe la FA.
Mashabiki wengi wamekuwa wakishinikiza uongozi wa timu hiyo ukae pembeni huku wengine wakitaja baadhi ya wachezaji wanahusika kwenye kuhujumu timu hiyo.
Hivyo Simba italazimika kushinda ili kurudisha hali ya mambo ndani ya klabu hiyo ikiwa pamoja na umoja uliokuwepo hapo awali.
CHANZO:BINGWA
0 comments:
Post a Comment