GABES,TUNISIA.
TP Mazembe imekuwa klabu ya kwanza kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika licha ya jioni ya leo kufungwa mabao 2-1na Klabu ya Stade Gabesien ya Tunisia katika mchezo wa marudiano uliochezwa huko Stade Olympique de Gabes,Tunisia.
Wenyeji Stade Gabesien ndiyo wakioanza kupata bao mapema kabisa dakika ya 28 tu ya mchezo kupitia kwa Youssef Fouzai.Fouzai alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penati uliopatikana baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi na kipa wa TP Mazembe Sylvain Gbohouo.
Dakika ya 69 TP Mazembe ilifanikiwa kupata bao la kusawazisha kupitia kwa Merveille Bope aliyeuwahi mpira wa kichwa wa Jonathan Bolingi.
Baada bao hilo wenyeji Stade Gabesien walikuja juu na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 74 kupitia kwa Ahmed Hosni.Hosni alifunga bao hilo baada ya kuwalamba chenga walinzi wawili wa TP Mazembe na kumfunga kirahisi mlinda mlango Sylvain Gbohouo.
Dakika ya 76 TP Mazembe ililazimika kucheza pungufu baada ya kiungo wake Jonathan Bolingi kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa mchezo usio wa kiungwana.
Kwa matokeo hayo TP Mazembe imefanikiwa kutinga hatua ya makundi kwa faidi ya bao la ugenini baada ya kushinda bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa huko Lubumbashi wiki mbili zilizopita.
0 comments:
Post a Comment