Dar es salaam,Tanzania.
RAIS wa klabu ya Simba, Evans Aveva amesema kuwa wamechoka kuchekwa
na watani wao wa jadi Yanga kutokana na kuboronga kwao msimu huu na
hivyo wanajipanga kufanya mapinduzi makubwa msimu ujao.
Simba imeshapoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania
Bara ambao umekwenda kwa Yanga, tena wakifanya hivyo wakiwa na mechi
tatu mkononi.
Kitendo hicho kimewafanya mashabiki wa Simba kutaniwa na watani wao
kwa kupewa majina lukuki kama ‘Wamatopeni FC’, ‘Chura FC’, ‘Wamchangani
FC’ na mengineyo kutokana na maelezo kuwa timu hiyo haina hadhi ya
kucheza michuano ya kimataifa.
Kwa upande wao, Yanga ambao kwa misimu minne sasa imekuwa ikishiriki
michuano ya kimataifa, mashabiki wake wamekuwa wakiiita timu yao
‘Wakimataifa’.
Ni kufahamu kudodora kwao huko kwa misimu minne sasa, Aveva anaamini
huu ni wakati wa kujipanga upya na kurejesha makali yao ya zamani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Aveva alisema kuwa kufanya kwao
vibaya msimu huu ndiyo mwisho kwani tayari wameandaa mipango madhubuti
ya kuijenga upya timu yao msimu ujao.
Aveva alisema kuwa wamejipanga kutumia kiasi kikubwa cha fedha wakati
wa usajili wa mwishoni mwa msimu huu ili kupata wachezaji wakali na
wenye uzoefu mkubwa.
Alisema shauku yao ni kuhakikisha msimu ujao wanatwaa ubingwa wa Ligi
Kuu Bara pamoja na kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa msimu
unaofuata.
“Tukiwa kama viongozi, tumekubaliana tufanye bmapinduzi ya hali ya
juu kwa kufanya usajili mzuri hali itakayotuwezesha kuhimili ushindani
wa ligi,” alisema.
Alisema kuwa kuanzia msimu ujao, wanataka kuwa na kikosi madhubuti
ambacho kitawapa ubingwa wa Bara, wakiamini kufanikiwa katika hilo
kutokana na fungu walilotenga.
Wakati ligi ikitarajiwa kufikia tamati Jumapili hii, Simba wana
pointi 62, wakipigania nafasi ya tatu dhidi ya Azam wenye pointi 63.
0 comments:
Post a Comment