Mbeya,Tanzania.
BAADA
ya mapumziko ya wiki moja kupisha wiki ya mechi za timu ya Taifa, Klabu
Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, inatarajia kuendeleza
kampeni yake ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL)
kwa kukipiga na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya
kesho saa 10.30 jioni.
Tayari kikosi cha Azam FC kipo kamili tokea juzi Jumapili kilipwasili
jijini hapa kwa ajili ya mchezo huo sambamba na ule wa Jumamosi ijayo
(Septemba 10) dhidi ya Mbeya City.
Kwa miaka mingi sasa tokea Azam FC ipande Ligi Kuu Julai 27, 2008,
imekuwa ikikutana na upinzani mkali kutoka kwa maafande hao katika mechi
zote za nyumbani na ugenini.
Rekodi zao (Head to Head)
Kuelekea mchezo huo wa kwanza wa ugenini wa Azam FC msimu huu, mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
umekuandalia rekodi muhimu za ligi tokea timu hizo zianze kukutana kwa
mara ya kwanza Oktoba 25, 2008, mchezo ulioshuhudiwa ndani ya Uwanja wa
Sokoine, Prisons ikishinda 2-0.
Mpaka sasa katika rekodi zao, Azam FC na Tanzania Prisons zimekutana
mara 12 ndani ya ligi, huku rekodi zao zikifanana kwenye kila kitu
kuanzia mechi za kushinda hadi walizotoka sare.
Rekodi hizo zinaonyesha kuwa, nusu ya mechi hizo 12 (mechi sita) timu
hizo zimeenda sare huku pia kila upande ukishinda mara tatu.
Jumla ya mabao 20 yamefungwa na timu hizo katika mechi zote 12
walizokutana, cha kustaajabisha zaidi kila timu imefunga mabao 10 jambo
ambalo linaongeza zaidi mvuto kwenye mchezo wa kesho.
Hadi timu hizo zinakutana tena, Azam FC imeonekana kuwa na takwimu
nzuri ya ufungaji mabao kuliko Prisons msimu huu, wakati wote wakiwa
wamecheza mechi mbili mpaka sasa matajiri hao wamefunga manne huku
maafande hao wakitupia mawili tu, lakini wote wameruhusu wavu wao
kuguswa mara moja.
Ukiondoa mechi za ligi, pia timu hizo zimewahi kukutana katika mechi
ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup)
Machi 31 mwaka huu ndani ya Uwanja wa Azam Complex, mchezo ambao uliisha
kwa Azam FC kuibuka kidedea kwa kufuzu kwa nusu fainali kwa ushindi wa
mabao 3-1, yaliyofungwa na Shomari Kapombe aliyetupia mawili na Khamis
Mcha akitupia moja.
Mfanano na msimu uliopita
Pambano hili limeonekana kufanana na lile la msimu uliopita kwenye
mzunguko wa pili kwa upande wa Azam FC, ambapo matajiri hao wataingia
dimbani wakiwa na lengo kubwa la kuibuka na ushindi ili kurejea kileleni
katika msimamo wa ligi.
Vilevile Februari 24 mwaka huu zilipokutana mara ya mwisho ndani ya
uwanja huo, Azam FC iliingia dimbani ikiwa na nia ya kuibuka na ushindi
ili kurejea kileleni kwa kuishusha Yanga, lakini ilishindwa kufikia
malengo hayo kufuatia mchezo kuisha kwa sare ya bila kufungana.
Hivyo, hata kesho ushindi wowote wa zaidi ya bao moja kwa upande wa
Azam FC, utaifanya kurejea kileleni kwenye msimamo ikifikisha pointi
saba na kuishusha Mbeya City ambayo nayo ina pointi hizo lakini
itazidiwa idadi ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa (GD) kwani
mpaka sasa imefunga mabao manne tu na kufungwa moja.
Bocco kuendelea kucheka na nyavu?
Nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, ameendelea kuwa mhimili
mkubwa kwenye eneo la ushambuliaji la timu hiyo, ambapo hadi sasa msimu
huu amefanikiwa kufunga mabao mfululizo katika mechi zilizopita za Azam
FC.
Mpaka sasa ameandika rekodi ya kufunga mabao matatu ndani ya mechi
mbili, akifunga moja kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya African Lyon
iliyoisha kwa sare ya 1-1 na akatupia mawili Azam FC ilipoichabanga
Majimaji ya Songea 3-0.
Bocco ambaye pia ni nahodha msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania
‘Taifa Stars’, mpaka sasa katika mechi za mashindano msimu huu, amefunga
mabao manne ndani ya mechi tatu.
Mechi nyingine iliyomfungulia rekodi hiyo ni ile dhidi ya Yanga
waliyoshinda kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani
ya dakika 90 na kutwaa taji la Ngao ya Jamii, ambapo Bocco alifunga bao
la pili la kusawazisha dakika ya 89.
Jambo kubwa linalosubiriwa kesho ni Je, Bocco ataendelea na moto
wake wa kutupia mabao zaidi na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa
wafungaji bora msimu huu? Ni jambo la kusubiri baada ya dakika 90
kumalizika.
Zeben alonga
Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, amewaambia mashabiki wa timu
hiyo kuwa wamekuja na kazi moja tu mkoani Mbeya kusaka pointi sita
wakianza na ushindi kwa mchezo wa kesho dhidi ya maaafande hao.
“Lakini izingatiwe ya kuwa ligi sio nyepesi kiasi hicho kutokana na
timu zote tulizocheza nazo kujiandaa, kikubwa tumekuja kufanya kazi
tutaonyesha uwezo wetu, lakini tunaamini kuwa tutahakikisha tunapata
zile pointi ambazo tumekuja huku kuzifuata na baada ya hapo tutarudi
nyumbani (Dar es Salaam) kucheza mchezo dhidi ya Simba,” alisema.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji murua kabisa
kinachochangamsha koo cha Azam Cola, katika kufanya maandalizi yake
mwisho kabla ya kupambana na Prisons, leo Jumanne jioni inatarajia
kufanya mazoezi ya mwisho ndani ya uwanja huo ikiwa na kikosi chake
kamili.
0 comments:
Post a Comment