Manchester,England.
MENEJA mpya wa Manchester City,Mhispania Pep Guardiola,ameendelea kukiongezea sura mpya kikosi chake hii ni baada ya Jumamosi Usiku kuinasa saini ya Straika wa Colombia Marlos Moreno kutoka klabu ya Atletico Nacional.
Moreno,19,amesaini mkataba wa miaka mitano na inasemekana Manchester City imetumia kitita cha Paundi 4.75 Milioni kumpata.
Taarifa zaidi zinasema Manchester City haitamtumia Moreno msimu huu na badala yake itatamtoa kwa mkopo kwenda klabu ya Deportivo La Coruna ya Hispania ili kupata uzoefu wa soka la Ulaya.
Moreno anakuwa mchezaji wa saba kujiunga na Manchester City katika kipindi hiki cha usajili barani Ulaya baada ya Leroy Sane,Ilkay Gundogan, Nolito, Oleksandr Zinchenko,Gabriel Jesus na Aaron Mooy.
Moreno ameichezea Colombia jumla ya michezo saba na alikuwa sehemu ya kikosi cha nchi hiyo kilichofika nusu fainali ya michuano ya Copa America Centenario iliyofanyika nchini Marekani ambapo alicheza michezo minne na kufunga bao moja.
Mapema mwaka huu,Moreno,aliisaidia Atletico Nacional kutwaa ubingwa wa Copa Libertadores na amejizolea sifa nyingi nchini kwao Colombia huku kiuchezaji akifananishwa na staa wa zamani wa nchi hiyo,Faustino Asprillia.
0 comments:
Post a Comment