London,Uingereza.
USAJILI wa Shkodran Mustafi kwenda Arsenal kwa dau la £35m siyo kwamba umeonyesha kuwa klabu hiyo imeanza kuondokana na ubahili bali pia umefanya vilabu vya ligi kuu ya Uingereza kuweka rekodi mpya katika kipindi hiki cha usajili baada ya kutumia zaidi Paundi Bilioni 1 (£1,021,430,000) katika kipindi /dirisha moja la usajili.
Wiki iliyopita ligi kuu ya Uingereza tayari ilikuwa imevunja rekodi yake ya awali pale Manchester City ilipomsajili aliyekuwa kipa wa Barcelona,Claudio Bravo kwa dau la £17m.
Usajili huo ulifanya pesa ambayo imetumiwa katika usajili kwa dirisha hili pekee kufikia £880m na kuvuka £870m iliyotumiwa katika usajili wote wa dirisha lililopita.Huu ni msimu wa nne mfululizo vilabu vya Uingereza vinavunja na kuweka rekodi mpya katika usajili.Pesa hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi kwani bado kuna siku moja zaidi ya vilabu kufanya manunuzi.
Wakati huo huo Hull City imekuwa klabu ya12 kuvunja rekodi yake ya usajili msimu huu pale ilipomsajili kiungo Ryan Mason kutoka Tottenham kwa ada ya £11m.Kabla ya hapo vilabu 11 msimu vilikuwa tayari vimevunja rekodi zao zenyewe vikiongozwa na Manchester United iliyovunja rekodi yake kwa kumsajili kiungo Paul Pogba kutoka Juventus kwa ada ya £89m.
0 comments:
Post a Comment