KOCHA wa Yanga, Hans van Pluijm amesema atatumia Ligi Kuu Bara kama maandalizi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Akizungumza jana Pluijm alisema kilichowaangusha kwenye
michuano ya msimu huu ni wachezaji wake kukosa uzoefu lakini kwa sasa
wameshaiva hivyo mwakani anatarajia kufanya vizuri zaidi.
“Mwakani sitaki tena kushuka na kucheza shirikisho, lengo langu ni
kuhakikisha tunafanya vizuri klabu bingwa na kucheza hatua ya nane bora
na si vinginevyo, kilichotufanya tukashuka shirikisho ni wachezaji wangu
kukosa uzoefu,” alisema Pluijm.
“Tulikosa uzoefu, tukajikuta tunafungwa hata nyumbani, ilipaswa
kupata ushindi kwenye mechi za nyumbani, pia tulifanya makosa mengi
kwenye safu yetu ya ulinzi na hiyo ndiyo ilitufanya tufungwe mabao
ambayo mengine ni ya kizembe… “Kiukweli mechi za nyumbani ni lazima
ushinde, usipofanya hivyo kwako unadhani utawezaje ugenini, tayari
nimeshaongea na wachezaji wangu kusahau yaliyopita, tujipange kwa
kutetea ubingwa na hapo hapo tutumie ligi kujinoa zaidi kwa ajili ya
klabu bingwa mwakani,” alisisitiza.
“Nitatumia michuano ya Ligi kama moja ya maandalizi ya michuano ya
klabu bingwa mwakani na pia kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu,”
alisema.
Yanga itaanza harakati zake za kutetea ubingwa huo katika mchezo
dhidi ya African Lyon kesho kutwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Yanga ilifungashiwa virago na Al
Ahly ya Misri baada ya kuchezea kichapo cha mabao 2-1 wakiwa ugenini na
kuangukia kucheza Kombe la Shirikisho ambalo nalo wameshatupiwa virago.
Kabla ya mchezo wao wa mwisho dhidi ya TP Mazembe ambayo walikula
kichapo cha mabao 3-1 mapema wiki hii, Yanga ilikuwa tayari imeshacheza
mechi tano dhidi ya MO Bejaia, Medeama na TP Mazembe na kufungwa tatu,
sare moja na kushinda moja, ikikusanya pointi nne.
0 comments:
Post a Comment