728x90 AdSpace

  • Latest News

    Wednesday, August 24, 2016

    MAKALA:HUYU NDIYE JOSEP “PEP” GUARDIOLA.


    Joe Hart na Pep Guardiola


    Na Chikoti Cico.

    Ni fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya kati ya Manchester United dhidi ya Barcelona jijini London ndani ya uwanja wa Wembley, dakika ya mchezo ni 86 na sekunde ya 15 na ubao unasomeka Barcelona wanaongoza kwa magoli 3-1.

    Na ndipo kamera za uwanja zikafika kwenye mikono ya kocha wa Manchester United wakati huo Sir Alex Ferguson, sio kwamba pete yake ya ndoa ilikuwa imeng’aa sana kiasi cha kupendwa na kamera bali ni kutetemka kwa mikono yake ndiko kulikoleta macho ya kamera karibu.

    Kocha wa Barcelona wakati huo Pep Guardiola ndiye aliyesababisha kutetemka kwa mikono ya kibabu Ferguson, ni siku hiyo ndipo kilele cha tiki-taka na utatu mtakatifu wa Messi-Xavi-Iniesta chini ya Guadiola ulipoifanya dunia isimame kwa sekunde kadhaa.

    Na Barcelona ikanyakua kombe la ligi ya mabingwa Ulaya chini ya Guardiola kwa mara ya pili na dunia nzima ikaujua umahiri, ujuzi, utaalamu na ufundi wa kocha huyo Mhispania ambaye kwasasa ni kocha mkuu wa Manchester City.

    Pamoja na umahiri, ujuzi, utaalamu na ufundi huo alionao pia kuna upande wa pili wa Guardiola ambao wengi hawaufahamu, upande ambao kocha huyu hufanya lolote bila kujali chochote kwaajili ya kuifanya filosofia yake iweze kutimia ndani ya klabu yoyote ile afundishayo.



    Joe Hart akiwa benchi


    Baada ya kupewa kuiongoza klabu ya Barcelona cha kwanza kabisa alichokifanya ni kuwaondoa kikosini wachezaji ambao kocha huyo aliamini kwamba hawataweza kuendana na mfumo wake, wa kwanza kabisa alikuwa ni Ronaldinho Gaucho, mchezaji ambaye uwanja mzima wa Barcelona; Nou Camp ulimuimba mchezaji ambaye dunia ilimuimba ila Pep hakujali akamwondosha Mbrazili huyo na ufundi wake.

    Ronaldinho na Deco ambao walikuwa wachezaji mahiri na muhimu chini ya kocha Frank Rijkaard na ambao waliipa Barcelona ubingwa wa ligi ya mabingwa Ulaya mwaka 2006 wote walifungasha virago chini ya Guardiola.

    Na hata alipofika Bayern Munich mchezaji nguli na gwiji wa klabu hiyo Bastian Schweinsteiger naye aliondoshwa klabuni hapo ambapo Guardiola aliamini kwamba kiungo huyo hawezi kumpa kile akitakacho kwenye mfumo wake bila kujali kama huyu ni mtumishi mwaminifu wa Bayern Munich.

    Kwahiyo kinachomtokea kwasasa kipa mahiri na mchezaji wa muda mrefu ndani ya klabu ya Manchester City; Joe Hart sio jambo geni na sababu kubwa ikiwa ni kwamba Hart hawezi kuichezesha timu kutokea eneo la nyuma, yaani upigaji na ugawaji wake wa mipira ni dhaifu kuweza kuendana na mfumo wa kocha huyo.

    Mbele ya Guardiola kazi ya kipa ya kwanza ni kuanzisha mashambulizi kutokea eneo la nyuma tofauti na ilivyo kawaida kwamba kazi ya kipa ni kuzuia michomo isiingie golini.

    Na ndiyo maana takwimu za kipa wa Bayern Munich Manuel Neuer chini ya Guardiola zinaonyesha tofauti ya kati ya kuongezeka kwa upigaji pasi na kupungua kwa uzuiaji michomo, msimu wa 2013/14 Pasi- 872, kuzuia michomo- 72, 2014/15 pasi- 1,072, kuzuia michomo- 69, 2015/16 pasi- 1,111, kuzuia michomo- 63.

    Alipoulizwa swali na waandishi wa habari kuhusu kumuweka benchi Hart, pamoja na maneno mengine Guardiola alisema “…… niko hapa Manchester City kwasababu waliwasiliana nami ili kufundisha vile nnavyopenda…….” Hayo ni maneno ya kocha ambaye kwa namna yoyote ile atafanikisha falsafa yake.

    Joe Hart nafasi yake Manchester City itachukuliwa na Bravo ambaye anakaribia kukamilisha usajili wake kutokea Barcelona na hivyo kuthibitisha kuondoka kwa Hart ama kukalia benchi, mbele ya makocha wengine Hart ni kipa mahiri lakini sio Guardiola.

    Na huyo ndiye Guardiola ambaye ukiachana na falsafa ya tiki-taka iliyompa jina na umaarufu duniani pia ni kocha ambaye ana misimamo yake katika kukitetea kila anachokiamini bila kujali chochote wala yeyote.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: MAKALA:HUYU NDIYE JOSEP “PEP” GUARDIOLA. Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top